2018-03-08 16:13:00

Shuhudieni imani yenu kwa matendo ya mwanga, alama ya maisha mapya!


Mungu amemuumba mwanadamu kusudi aunganike naye milele. Hii ni kwa sababu ya upendo wake mkubwa usio na mwisho. Mwanadamu anapoingia katika hali ya uasi Mungu anaendelea kumfikiria na kumtafuta. Pamoja na kwamba wakati mwingine Mungu humwadhibu mwanadamu kwa sababu ya uovu wake, hukumu yake haiushindi upendo wake. Ndiyo maana Mama Kanisa anatupatia fursa kila mwaka ya kupita katika kipindi cha toba kusudi kustahilishwa kushirikishwa furaha ya upendo wake. Antifona ya Mwanzo ya Dominika hii inayoitwa Dominika ya Furaha inatualika katika furaha hiyo ikisema: “Furahi Yerusalemu: mshangilieni ninyi nyote mmpendao: furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake”. Tunaalikwa kufurahi sababu katika Yeye tutafarijiwa, tutanyonya maziwa na kushibishwa, ishara ya kuwa hai tena.

Somo la kwanza linatuonesha kuwa hukumu ya Mungu ni ya haki sababu ya uovu wetu; haki ya Mungu ndiyo huruma yake, ufunuo wa upendo wake usio na kikomo kwani wema wake haushindwi na uovu wa mwanadamu. Dhambi zetu haziufifishi wema wake wala kumfanya Yeye kukata tamaa. Hii ni kwa sababu upendo wake mkuu wadumu milele. Mwenyezi Mungu aliwatumia wakuu wa watu na makuhani wa taifa ya Israeli wajumbe ili kugeuza mienendo yao “kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake; lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake; na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponywa”.

Mwanadamu katika hali ya uhasi mkuu hivi anatangaziwa wokovu wa Mungu kupitia Koreshi mfalme wa Uajemi. Hapa ndipo urefu na upana wa upendo wa Mungu unapojidhihirisha. Maneno yake kupitia kinywa Nabii anasema: “Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? … si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake akaishi?” (Ezek 18:23). Mungu afurahii hali yetu ya uovu. Hii ni kwa sababu sisi tulio matunda ya kazi yake njema ya uumbaji ametuumba tukiwa wakamilifu na wenye sura na mfano wake. Hali ya dhambi inatuziba na kushindwa kuionesha haiba hii; inaturubuni tuache kuutangaza ukuu wa Mungu unaofichika ndani mwetu.

Kilele cha upendo wake huu mkuu ni katika nafsi ya Kristo, mwanaye mpendwa, Nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu sana. Yeye analetwa kwetu kama njia ya wokovu ambayo kwayo wote watakaomwamini wataokolewa. Kristo anaonesha namna ya kuujongea wokovu huo. Anamwambia Nikodemo katika somo la Injili: “Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye”. Mwana wa Adamu atainuliwa juu msalabani ishara ya wokovu wetu. Tendo hili la kuinuliwa kutoka katika ardhi ni ishara ya kuinua macho ya mioyo yetu kutoka katika kawaida ya maisha ya dunia hii na kwenda juu.

Kuwa juu ni ishara ya kuungana na Mungu na kuyatazama malimwengu katika jicho la kimungu. Hiyo ndiyo imani ambayo Kristo anatualika tuwe nayo katika Yeye. Maisha yake ya hadharani hapa duniani yametufunulia namna mbalimbali za kuyakabili maisha katika jicho la Mungu. Ni wazi kwamba namna hiyo kwa walioangalia katika jicho la kidunia waliona ni chukizo kiasi cha kumwadhibu kwa namna hiyo ya kikatili. Lakini namna yao ya kumwadhibu kwa kumwinua juu ya msalaba ni sababu ya wokovu wetu na ufunuo wa upendo wa Mungu kwetu. Tunapoelekeza macho yetu katika msalalaba na kuungana naye huku tukiyaangalia malimwengu kutoka juu tutapata nguvu ya kupita katika ulimwengu kinzani huku tukielekea kwa Mungu.

Injili Takatifu inataadharisha pia juu ya upande wa pili, yaani kwa wale wasioamini. Neno la Mungu linasema: “asiyeamini amekwisha hukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu”. Asiyeamini ni yeye ambaye hapandi pamoja na Mwana pekee wa Mungu juu msalabani na kuyaangalia mambo katika namna ya Mungu. Huyu ni yule ambaye anatawaliwa na mienendo ya ulimwengu mamboleo ambao unaendelea kumpatia mwanadamu mwenye ukomo wa uelewa matumaini bandia juu ya ujuzi wake. Hukumu inamjia kwa sababu “nuru imekuja ulimenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu”. Mwanadamu anayeacha kumtazama Yeye aliyeinuliwa juu msalabani anaishia katika giza kwa sababu anabaki katika ukomo wa kuona ukweli wote.

Mwanadamu ana ukomo katika uelewa wake. Hivyo, ni pale tu mwanadamu anapounganika na Mungu mwenye uwezo wa kujua na kuona yote ataweza kufanikiwa. Leo hii tunashuhudia jamii ambayo haitaki kuinua macho juu na kuyaelwa yote katika muono wa kimungu. Matokeo yake tunakuwa ni kizazi chenye uelewa nusunusu wa mambo mbalimbali yamhusuyo mwanadamu. Masuluhisho mengi hufanyika nusunusu na wakati mwingine kutawaliwa na ubinafsi au kutafuta maslahi ya mtu mmoja mmoja. Kila mmoja anakuwa ni mjuaji na matokeo yake ni mafarakano na kutoelewana kati yetu. Hatuwezi kamwe kutoka katika hali hii kama tusipoitazama hii nuru inayotuzukia katika Yeye aliyeinuliwa juu msalabani.

Mtume Paulo anatukumbusha haiba yetu kwamba “tumeokolewa kwa neema”. Hali hii ya neema inatutenga na ulimwengu na kutuunganisha na Kristo aliyeinuliwa msalabani. Ni zawadi ya Mungu kwetu anayotupatia bila hata kustahili. Hii ni kwa sababu hata tulipokuwa katika hali ya dhambi kwa mastahili yetu “alituhuisha pamoja na Kristo”. Sakramenti ya ubatizo inatupatia uzima mpya. Tunazaliwa mara ya pili na kujazwa neema ya Mungu ndani mwetu, neema ambayo inatufanya kuwa wana warithi wa Mungu. Mwitikio wetu unapaswa kuwa ni shukrani kwa Mungu. Mzaburi anatuonesha namna njema ya kushukuru kwa njia ya kuyakumbuka matendo ya Mungu. Israeli alipokumbuka hali yake akiwa utumwani Babeli na hali yake ya sasa katika uhuru anaimba kwa shukrani akisema: “Ulimi wangu na ugandamane na kaakaa la kinywa  changu, nisipokukumbuka”

Majira ya Kwaresima ni fursa nyingine kwetu ya kubadili mwelekeo wa maisha kwa ajili ya wokovu wetu sote. Tuikumbuke aiba yetu kwamba tumeinuliwa juu kutoka katika ulimwengu huu. Ni kipindi ambacho tunaalikwa kuyainua macho yetu juu na kuelekeza kwa Mungu kwa kumtazama Yeye waliyemchoma. Kwake tunaweza kumwona Mungu ambaye amejinyenyekesha katika namna ya ajabu kwa ajili ya wokovu wangu mimi na wewe. Msalabani anatufundisha unyenyekevu, msamaha, utii, uvumilivu na zaidi ya yote upendo fadhila ambazo kwazo zinaimarisha mahusiano yetu na Mungu na pia mahusiano yetu sisi kwa sisi. Tendo letu la kumtazama Kristo msalabani litaufunua upendo wa Mungu na hivyo tunafanywa kuwa sababu ya wokovu kwa ulimwengu wote. Upendo wa Mungu kwetu ni mkubwa mno na kamwe haushindwi wala kufifishwa na uovu wa mwanadamu.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.