Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Mpango mkakati wa saa 24 kwa ajili ya Bwana, muda wa kukesha na Kristo

Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana ni muda muafaka wa sala, tafakari na upatanisho kwa Mungu na jirani ili kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu na vyombo vya uinjilishaji wa kina! - REUTERS

08/03/2018 15:00

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 9 Machi 2018, kuanzia saa 11: 00 jioni kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada Upatanisho wa ujumla, itakayofuatiwa na maungamo na maondoleo ya dhambi ya mtu mmoja mmoja kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa kwenye  Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Misericordiae vultus” yaani  “Uso wa huruma” kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima. Kila Jimbo linapaswa kufanya maadhimisho haya ili kuwapatia waamini nafasi ya kuweza kuchunguza dhamiri zao, kujuta, kuungama na hatimaye kutimiza malipizi, ili kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao, kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wa Mungu kwa binadamu. Kwa njia hii, waamini nao wanapaswa kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao  

Hii ni huruma inayopaswa pia kushuhudiwa katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho inayogusa undani wa mtu, kwani hili ni chimbuko la amani na utulivu wa ndani. Ni huruma inayosamehe na kuokoa. Mapadre waungamishi wanao wajibu wa kuwa ni watumishi waaminifu wa huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu, kwa kuwapokea waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma katika mfano wa Mwana mpotevu! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hata mwaka huu, Makanisa sehemu mbali mbali za dunia yataendelea kubaki wazi ili kutoa nafasi kwa waamini kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao katika Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja kwa mara nyingine tena huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Mahakama ya huruma ya Mungu.

Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika mahojiano maalum na Vatican News anapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kulikumbuka tena Kanisa kuhusu “Fumbo la la huruma ya Mungu”, chemchemi ya furaha, utulivu na amani na kwamba, hii ni sheria msingi inayojikita katika moyo wa binadamu, tayari kuanza safari ya toba na wongofu wa ndani, ili kuungana tena na Mwenyezi Mungu, kiini cha matumaini mapya.

Askofu Msonganzila anasema kwamba Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” tayari unatekelezwa Jimboni Musoma, kwani kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mama wa Mungu, Jimbo Katoliki Musoma, kuna kikanisa kwa ajili ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wa masaa 24. Lengo ni kuendelea kukesha pamoja na Kristo Yesu kama sehemu ya mchakato wa majibu endelevu kutoka kwa waamini mintarafu swali la Kristo Yesu, Je, Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni muombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi ila mwili ni dhaifu! Rej. Mk. 14 37- 38. Yesu katika maisha na utume wake, alipenda kujitenga na malimwengu ili kuweza kufanya maamuzi mazito katika maisha yake. Alifunga na kusali kwa muda wa siku arobaini jangwani; akafunga na kusali kabla ya kuwachagua mitume wake, akasali kiasi cha kutokwa matone ya damu alipokuwa anajiandaa kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake.

Kumbe, Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” ni muda muafaka hata kwa waamini kujitenga kidogo na malimwengu ili kutafakari kuhusu maisha na wito wao kwa: kusali, kuabudu, kuomba, kushukuru, kusifu na kutukuza na hatimaye, kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Haya, kimsingi ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali!

Askofu Michael Msonganzila anakaza kusema, huruma ya Mungu inapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu, ufunuo halisi wa Uso wa huruma ambaye alisimika Ekaristi Takatifu kama ukumbusho wake wa milele na sadaka yake ya Pasaka. Ndiyo maana waamini wanaalikwa kumkazia tena na tena macho ya imani katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Ni muda muafaka wa kuabudu, kusali, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kujipatanisha na Mungu. Ikumbukwe kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni mahali pa pekee sana ambamo huruma ya Mungu inaadhimishwa. Hapa waamini wanatakatifuzwa, tayari kwenda kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya mwanga na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili.

Askofu Msonganzila anaendelea kufafanua kwamba, Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” ni suala mama katika maisha na utume wa Kanisa, kumbe, linapaswa kuvaliwa njuga ili liweze kuwa ni endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Mpango huu unaweza kumwilishwa katika kila Parokia, walau mara moja kwa mwezi ili kuleta roho ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani; roho na ari ya kutaka kukuza na kudumisha utume wa Sala na Biblia kwa kukesha na kusali. Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma anahitimisha mahojiano maalum na Vatican News kwa kusema, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo, zawadi ya Kristo kwa waja wake; ni chakula cha maisha ya uzima wa milele na kwamba, hili ni Fumbo linalopaswa kutangazwa na kushuhudiwa, tayari kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

08/03/2018 15:00