Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

ICMC: Miaka 65 ya huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani!

Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji kwa Miaka 65 imejizatiti kuwahudumia na kuboresha maisha ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia.

08/03/2018 15:14

Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji ICMC, ilianzishwa na Papa Pio XII ili kujibu kilio cha mahangaiko ya watu, kufuatia athari kubwa za Vita kuu ya Pili ya Dunia na Katiba yake ikapitishwa kunako mwaka 1951. Kwa sasa Tume hii inaongozwa na Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, Kenya, kama Rais wake, ili kusaidia mchakato wa kuwahudumia wahamiaji sehemu mbali mbali duniani!

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 8 Machi 2018 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume hii kwa kusema kwamba, Kanisa linatambua mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji ni sehemu pia ya mahangaiko ya Kristo Yesu na Kanisa lake, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli katika Agano la Kale. Mwenyezi Mungu anayaona mateso ya watu wake na anayafahamu maumivu yao na kwamba, anapenda kuwaokoa! Ili kutekeleza azma hii, Mwenyezi Mungu akamteua na kumtuma Musa ili kuwapangusa machozi na kuwapatia tena matumaini. Utume kama huu, umetekelezwa na Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji, katika kipindi cha miaka 65 iliyopita kwa kujipambanua kwa njia ya huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani:  “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii inamwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na aina mbali mbali ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima yao.

Uzoefu na mang’amuzi ya Tume hii unaweza kuyasaidia Mabaraza ya Maaskofu na Majimbo kujipanga ili hatimaye, kuweza kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama ilivyokuwa kwa Mwenyezi Mungu aliyemtuma Musa kuwakomboa watu wake kutoka utumwani Misri. Ili kutekeleza dhamana na utume huu katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuwashirikisha: uzoefu, mang’amuzi na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji duniani, ili kila upande uweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa Wahamiaji, maarufu kama "Global Compact", ni sehemu ya maboresho makubwa yanayovaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa katika maboresho ya usalama wa wahamiaji; mahali muafaka pa utekelezaji wa majadiliano haya. Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji, ICMC., imekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuragibisha majadiliano haya ili kujibu kilio na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anayashukuru Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia ambayo yameanza kupiga hatua kuelekea huko; kwa kuonesha nia na ushuhuda wa pamoja wa utekelezaji sera na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji inayofanywa na Mama Kanisa. 

Kazi hii bado ni pevu sana, kumbe, kuna haja ya kuhamasisha Serikali mbali mbali kushirikiana kwa dhati ili kutoa majibu muafaka kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo. Utekelezaji huu unafumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa na kwamba, maneno yaliyowekwa kwenye Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa wahamiaji yanatekelezwa kwa vitendo kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa. Baba Mtakatifu anasema, lakini kazi ya Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji, ICMC., inapaswa kwenda mbele zaidi kwa kuwa ni shuhuda na chombo cha upendo wa huruma ya Mungu kwa wakimbizi na wahamiaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/03/2018 15:14