Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Achana na wanawake bwana! Utalala mlango wazi! Ni majembe ya nguvu!

Siku ya wanawake duniani kwa mwaka 2018 - AP

08/03/2018 15:52

Kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchango wa wanawake duniani, tangu pale haki zao msingi zilipoanza kutambuliwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii wanamoishi. Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini anasikitika kusema, katika jamii ambamo mfumo dume bado unatawala, mchango, dhamana na ushiriki wa wanawake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni kidogo sana. Matokeo yake ni “vipigo vya majumbani”, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; ukeketaji; ukosefu wa usawa katika fursa za ajira na malipo; uwakilishi mdogo katika kupanga na kutekeleza majukumu mbali mbali ya kijamii!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa halina budi kusoma alama za nyakati kwa kutambua mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa ambalo ni Mama na Mwalimu. Idadi ya wanawake wanaofanya utume wao mjini Vatican inaendelea kuongezeka maradufu, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kuwaheshimu na kuwaenzi wanawake; kwa kuwapatia nafasi katika kufanya maamuzi na utekelezaji wake! Kamwe wanawake wasiwe ni vichokoo vya kuridhisha tamaa za watu, kwa kuwatumbukiza katika utumwa mamboleo. Wanawake ni vyombo muhimu sana katika kurithisha imani, tunu msingi za maisha ya kifamilia, kiutu na kijamii!

Kutambua na kuthamini utu na heshima ya wanawake, kuna maanisha kwamba, wanawake wanao mchango mkubwa katika mchakato mzima wa maisha ya hadhara!  Kimsingi wanawake wamekirimiwa zawadi ya kufundisha, kuelimisha na kuwafunda watu! Upatanisho ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Kuna haja ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli waamini wa dini mbali mbali waweze kuheshimiana na kuthaminiana kwa kukuza na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa kweli. Mchakato huu pia hauna budi kuwagusa wanawake na wanaume ili waweze kujipatanisha, tayari kushirikiana katika kukuza na kudumisha upatanisho wa wote.

Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho, haki na amani duniani, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Stefano, Shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya imani kwa Kristo na Kanisa lake! Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa ni chachu ya majadiliano yaliyowagusa wale ambao kutokana na sababu mbali mbali, walikuwa wametengwa na jamii kama ilivyotokea kwa yule Mwanamke Msamaria pale kisimani. Kumbe, wanawake washirikishwe kikamilifu katika mchakato mzima wa majadiliano ya kidini katika ngazi mbali mbali duniani!

Kwa upande wake, Nuria Calduch-Benages, mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu kutoka Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian anafafanua kuhusu uzoefu wa wanawake katika makuzi na uelimishaji wa udugu ndani ya jamii mintarafu Maandiko Matakatifu kwa kuonesha mchango wa wanawake katika masuala ya kijamii, kisiasa na kisheria. Amekazia kwamba, hekima inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu ni chemchemi na chachu ya majadiliano ya kidini na kiekumene; chachu inayopaswa kusaidia mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Kitabu cha Hekima ya Sulemani, Zaburi na Mithali vinamwonesha mwanamke kuwa kama: mtoto, dada, kijana; mama, mwalimu, kiongozi, mwandani na mkarimu. Mwanamke daima anaoneshwa kuwa karibu sana na Mwenyezi Mungu. Mwanamke anaweza kusaidia mchakato wa kufunda watu udugu kwa kujikita katika: ukweli na uwazi; uaminifu; kwa kuwajengea vijana utamaduni wa kupenda haki, amani na maridhiano; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; lakini jambo la msingi ni kuwa mashuhuda na vyombo vya upendo na mshikamano wa kidugu! Wanawake wanayo nafasi na dhamana ya pekee kabisa, katika mchakato wa kukuza na kudumisha maendeleo endelevu ya binadamu; kwani mwanamke amekirimiwa na mapaji mbali mbali yanayoweza kusaidia kufikia malengo haya. Mwanamke hana tabia ya ushindani usiokuwa na tija wala mashiko; si mtu anayejikita sana katika ukiritimba kama ilivyo kwa wanaume wengi. Hekima inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu ni chemchemi na chachu ya majadiliano ya kidini na kiekumene; chachu inayopaswa kusaidia mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

08/03/2018 15:52