2018-03-07 15:43:00

Papa Francisko: Michezo inajenga umoja na kushinda ulemavu


Michezo ya Paralympic inayowashirikisha watu wenye ulemavu wa viungo huko mjini Pyeongchang, Korea ya Kusini, iliyokuwa mwenyeji wa mashindano ya Olympic yaliyohitimishwa hivi karibuni ni fursa nyingine tena ya kujenga na kudumisha misingi ya amani na mshikamano kati ya watu. Mashindano ya mwaka 2018 yameonesha kwamba michezo inaweza kuwa ni daraja ya kuunganisha mataifa ambayo yako kwenye ukinzani, na hivyo kuanza mchakato wa amani na maendeleo! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, kuhusu Ibada ya Misa Takatifu, Jumatano, 7 Machi 2017 mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya michezo, watu wenye ulemavu wanaweza kuvuka kikwazo hiki, kwa kuonesha na kushuhudia ujasiri, udumifu, ari na moyo wa kupambana na hali mbali mbali za maisha bila ya kukata wala kukatishwa tamaa na ulemavu wa viungo! Michezo ni shule muhimu sana inayowashirikisha watu wote, lakini kwa namna ya pekee kabisa ni changamoto kwa wanamichezo wenyewe kuratibu maisha yao pamoja na kujitwika dhamana ya kuleta mageuzi katika jamii! Mwishoni, Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia heri, baraka na mafanikio viongozi wa Kamati kuu ya Michezo ya Paralympic Kimataifa, wachezaji na viongozi wa Korea. Anapenda kuwahakikishia sala na sadaka yake katika mashindano haya ili kweli michezo iwe ni fursa ya kujenga amani na furaha kati ya watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.