2018-03-07 15:20:00

Papa Francisko: Kipindi cha Mageuzo ni kiini cha Ibada ya Misa!


Sala ya Ekaristi Takatifu ni sehemu muhimu sana ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ni kiini na utangulizi unaowawezesha waamini kuweza kushiriki Ekaristi Takatifu, kama alivyofanya Kristo Yesu, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, kwenye Karamu ya Mwisho, alipotwaa divai na mkate akashukuru, akaumega na akawapa wafuasi wake, kama kielelezo cha uwepo wake endelevu na ishara ya daima ya shukrani inayomwilishwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu linalowawezesha waamini kujishikamanisha na sadaka ya ukombozi.

Mama Kanisa katika Sala ya Ekaristi Takatifu anaelezea kile ambacho kinaadhimishwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na sababu ya maadhimisho haya yanayopania kujenga umoja na Kristo Yesu aliyemo kwenye maumbo ya mkate na divai! Padre anayeadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, baada ya kuwaalika waamini kuinua mioyo yao kwa Bwana, ili kumshukuru, Padre anasali sala ya Ekaristi Takatifu,  kwa sauti kubwa, kwa niaba ya waamini wote waliohudhuria katika Ibada hii, kwa kumshukuru Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu. Lengo kuu la Sala ya Ekaristi Takatifu ni kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kazi kubwa pamoja na kutolea Sadaka.

Hii ni sehemu ya Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Jumatano, tarehe 7 Machi 2018 kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi kuhusu Ibada ya Misa Takatifu. Ili kuweza kuadhimisha na kushiriki vyema Mafumbo haya ya Kanisa, waamini wanapaswa kuwa na uwelewa mpana zaidi na ndiyo maana Kanisa linayatamka maneno haya katika lugha inayofahamika na waamini hawa, ili kuweza kuunganika katika sala na shukrani zinazotolewa na Padre kiongozi wa Ibada. Sadaka ya Kristo na Sadaka ya Ekaristi Takatifu ni sadaka moja tu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Misale ya Altare kuna sala mbali mbali za Ekaristi Takatifu ambazo zinafumbata utajiri mkubwa wa amana na imani ya Kanisa. Utangulizi ni tukio la shukrani kwa zawadi mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia wanadamu, lakini zawadi kubwa ni ile ya kumtuma Mwanaye wa pekee, kuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Utangulizi unahitimishwa kwa waamini kusali au kuimba wimbo wa Mtakatifu Mtakatifu Mtakatifu Bwana Mungu wa majeshi. Hapa waamini wanaunganisha sauti zao na zile za Malaika pamoja na watakatifu ili kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Baadaye inafuata sala ya kuombea dhabihu ili ziweze kutakaswa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na kuwa ni Mwili na Damu ya Kristo Yesu. Nguvu ya Roho Mtakatifu inatenda kazi kwa njia ya Padre, kiongozi wa Ibada, kwa njia ya maneno yaliyosemwa na Kristo Yesu, mkate na divai vinageuka kuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kwa mageuzo ya mkate na divai hufanyika mabadiliko ya uwamo wote wa mkate na divai katika uwamo wa Mwili wa Kristo, Bwana, kielelezo cha Sadaka ya Kristo Yesu Msalabani!  

Fumbo la Imani linawasaidia waamini kuweza kumwona Kristo Yesu katika maumbo ya mkate na divai. Kanisa linataka kujiunga na Kristo Yesu ili kuwa mwili mmoja na wale wote wanaoshiriki Fumbo hili la Ekaristi, ili nao pia waweze kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa katika ulimwengu mamboleo! Mama Kanisa anaunganisha sala na sadaka yake na ile ya Kristo Msalabani, mwaliko kwa waamini kuendeleza ari na moyo wa sala katika maisha yao kama walivyokuwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo, wakati ule Mtakatifu Petro alipokuwa amekamatwa na kutiwa gerezani.

Ikumbukwe pia kwamba, Ekaristi ni sadaka ya Kanisa. Kama Kristo alivyopanua mikono yake Msalabani, kwa njia yake, pamoja naye na ndani yake, Kanisa hujitoa na kuomba kwa ajili ya watu wote. Kanisa linamwomba Mwenyezi Mungu kuwakusanya watoto wake wote katika utimilifu wa upendo na Baba Mtakatifu, Askofu wanaotaja kwa majina pamoja na watumishi wake wote, kielelezo cha umoja wa Kanisa la kiulimwengu na Kanisa mahalia. Kanisa linawakumbuka na kuwaombea waamini walio hai na wale waliotangulia kwenye usingizi wa amani, wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu. Kanisa linamsifu na kumtukuza Mungu pamoja na Bikira Maria mwenye heri. Hii inaonesha kwamba, katika sala hii hakuna hata mtu mmoja ambaye anasahauliwa.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wakati wa sala hii ya Kanisa kuwakumbuka na kuwaombea ndugu, jamaa, marafiki na marehemu wao! Misa Takatifu ni Sadaka ya Kristo Msalabani inayotolewa kwa ajili ya wengi. Waamini wanahamasishwa kutoa sadaka kwa ajili ya kuwaombea ndugu zao, lakini, ikumbukwe kwamba, Sadaka ya Misa Takatifu haiuzwi kamwe! Waamini wajitaabishe kuyafahamu Mafumbo ya Kanisa ili waweze kuyaadhimisha vyema kwa ushiriki mkamilifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mambo msingi ya kuzingatia ni: Kumtolea Mungu shukrani, daima na mahali popote pale! Pili, waamini wahakikishe kwamba, maisha yao yanakuwa ni kielelezo cha zawadi ya upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu; hii ni zawadi huru na haina malipo hata kidogo! Tatu, waamini wahakikishe kwamba wanajenga na kudumisha umoja wa Kanisa. Sala ya Ekaristi Takatifu ni Katekesi makini na kiini cha Ibada ya Misa Takatifu. Ekaristi Takatifu ni zawadi ya neema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.