Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Mashuhuda wa utunzaji bora wa mazingira duniani wanavyopukutika!

Mashuhuda wa utunzaji bora wa mazingira wanaendelea kupukutika kutokana na vita ya ukoloni mamboleo inayoendeshwa kichini chini! - AP

07/03/2018 07:29

Takwimu za Taasisi isiyo ya serikali ya Mashuhuda wa Ulimwengu, Global Witness, zinaonesha kwamba tangu mwaka 2002 kila juma kuna watu wawili wanauwawa sababu ya kutetea Mazingira, lakini kwa mwaka 2016 na mwaka 2017 mauaji hayo yameongezeka maradufu na hivyo kufikia 200 kwa mwaka 2016, na mauaji 197 kwa mwaka 2017. Wahanga hawa wa utetezi wa mazingira wameanza kufahamika kama “Wafiaimani wa Mazingira”, Martyrs of the Earth, kwa sababu wanatafutwa na kuuwawa ili kuvunja nguvu ya utetezi wa utunzaji bora mazingira Nyumba ya wote, sambamba na Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Laudato sì, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.”

Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira  Laudato sì, ni changamoto kubwa katika uwajibikaji wa kijamii ili kulinda, kutunza na kuendeleza kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kwake na Mwenyezi Mungu. Kushindwa kutekeleza dhamana hii ni kutaka kuwatumbukiza watu katika maafa na majanga ya maisha na kwamba, waathirika wakuu ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.  

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya Barua hiyo ya kitume Laudato sì, juu ya utunzaji wa mazingira Nyumba ya wote, mnamo tarehe 20 Oktoba 2014 katika kikao na wawakilishi wa vyama vya kiraia, alitoa hotuba akiaalika washiriki na wote wenye mapenzi mema kuzingatia: utunzaji bora wa mazingira Nyumba ya wote, unaotoa fursa kwa wanadamu wote kujipatia mahitaji yao msingi; makazi kwa ajili ya kujihifadhi na hasa maskini na wahitaji; na ajira zenye kujali haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Katika kikao hicho, alishiriki pia Bi Bertha Caceres wa Honduras, ambaye mwaka 2015 alitunukiwa Tuzo ya Mazingira ijulikanayo kama Goldman Environmental Prize. Bi Bertha alikuwa mpigania haki za wazawa wa Honduras mintarafu utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya wakazi wa Honduras. Baada ya vitisho vingi, mnamo tarehe 3 Marchi 2016 aliuwawa nyumbani kwake na wavamizi wasiojulikana, waliokuwa na silaha.

Hivi karibuni huko Kenya, Bwana Esmond Bradley Martin, mwanajiografia wa Marekani na ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kupinga biashara haramu ya vipusa, aliyekuwa akiishi nchini Kenya kwa takribani miaka 30, amakutwa kauwawa nyumbani kwake Nairobi, akiwa na umri wa miaka 76. Hii ni vita baridi inayomwaga damu ya wanyonge wengi hasa wakazi wa maeneo yenye ardhi, madini, misitu, wanyama na rasilimali zingine asilia ambapo wafanyabiashara haramu wasiojali hali za wengine, na wanafanya kila namna kuharibu mazingira kwa faida zao binafsi. Vita hii inaonekana kuwa kubwa zaidi huko Amerika ya kusini hasa maeneo ya Amazonia ambako wafanyabiashara "waliokata mishipa ya aibu wamekodolea macho kodo" madini na sekta ya kilimo na kupelekea mauaji ya takribani asilimia 60 ya wapigania haki na utunzaji bora wa mazingira. Kwa mwaka 2017, huko Brazil taarifa zinaonesha wanyonge 46 wameuwawa, Colombia ni 32, na Mexico ni 15. nchi zingine waathirika wa vita hii baridi ya mazingira ni Guatemala, Nicaragua, Honduras na Perù.

Mabara ya Afrika na Asia pia ni wahanga wa mapambano haya yanayopelekea umwagaji wa damu ya wanyonge wengi. Huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Watu wa Congo ni mauaji 13 kwa mwaka 2017, ya wapigania utunzaji wa mazingira, wakati Ufilipino ni wameuwawa 41. Vita hii ni ngumu na ya hatari kubwa kwani wauaji hata wakikamatwa mara nyingi huachiwa huru bila adhabu na waliomstari wa mbele kutetea utunzaji wa mazingira wanajikuta wapo wapweke na kuishia kuuwawa. Hii ni ishara wazi kwamba washiriki wa uhalifu huo wametapakaa kwenye Nyanja zote hata serikalini na kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.

Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 21 Januari 2018, akiwa katika hija yake ya kitume nchini Perù, na kupata nafasi ya kutembelea eneo la Puerto Maldonado, aliweka msisitizo wa kufanyia kazi Barua yake ya Kitume Laudato sì, inayofundisha umuhimu wa utunzaji wa ekolojia, unaoitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu na kwa namna ya pekee, haki za watu mahalia kama vile huko Amazonia, ambako ukoloni mamboleo unaofumbatwa katika nguvu ya kiuchumi unatishia usalama, ustawi na maendeleo ya wengi.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

 

07/03/2018 07:29