2018-03-07 15:00:00

Kardinali Parolin: Kanisa litaendelea kuwahudumia wakimbizi!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani:  “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapoea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Haya ni mambo ambayo yamedadavuliwa kwa kina na  mapana katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018.

Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, huu ndio msimamo wa Kanisa na Vatican itaendelea kusimamia misingi hii kama sehemu ya sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji. Jumuiya ya Ulaya haina budi kuwacha malango ya mipaka yake wazi, ili kuwapokea wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kuliko walikotoka. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusoma alama za nyakati sanjari na kuendelea kuelimishana ili kweli wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji lisiwe kero, bali baraka na madaraja ya watu kukutana na kusaidiana! Kardinali Parolin ameyasema haya, wakati wa mahojiano maalum na Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, SIR, kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Italia na athari zake katika mchakato mzima wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya familia ya Mungu nchini Italia. Mama Kanisa ataendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu sanjari na kukazia mshikamano wa upendo kati ya watu wa Mataifa.

Kardinali Parolin anawataka waamini, watu wenye mapenzi mema pamoja na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, kuendelea kutoa huduma yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji na kwamba, watu hawa ni rasimali inayopaswa kuheshimiwa na kuendelezwa na wala si watu wa kubezwa, kunyanyaswa na kupuuzwa kamwe! Kuna haja ya kuendelea na kampeni ya uragibishaji wa changamoto ya wahamiaji katika mwelekeo chanya, badala ya kuwajengea hofu, mashaka na wasi wasi usiokuwa na mashiko wala mvuto kutokana na sababu za kisiasa! Pamoja na changamoto zote zilizopo: usalama wa raia na mali zao; rasilimali fedha na miundo mbinu ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi! Familia ya Mungu nchini Italia isiafungie milango wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama baada ya kukumbana uso kwa uso na majanga asilia pamoja na mtutu wa bunduki katika nchi zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.