2018-03-07 15:00:00

Jengeni utamaduni wa upendo na mshikamano na maskini!


Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji ICMC, ilianzishwa na Papa Pio XII kufuatia athari kubwa za Vita kuu ya Pili ya Dunia na Katiba yake ikapitishwa rasmi kunako mwaka 1951, ili kusaidia mchakato wa kuwahudumia wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia kwa kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa, kama vile: Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR pamoja na Mashirika ya Kiraia. Tume hii inashirikiana kwa karibu sana na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao wana: utu, heshima na utambulisho wao kama binadamu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Kanisa linamtambua Kristo Yesu anayeteseka miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi, ustawi na maendeleo yao, kwa kutambua kwamba, ni watu wanao kimbia vita, kinzani na athari za mabadiliko ya tabianchi! Wakristo kwa kushirikiana na wadau mbali mbali duniani wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ukarimu na mshikamano wa upendo kwa wakimbizi na wahamiaji! Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuwa na wongofu wa mawazo potofu dhidi ya wakimbizi na wahamiaji, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana katika kukabiliana na changamoto za maisha, ili kutengeneza dunia inatìyosimikwa katika haki, udugu na mshikamano! Hii ni sehemu ya hotuba ya ufunguzi wa Mkutano mkuu wa Mwaka wa Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Wahamiaji ICMC, ulioanza rasmi mjini Roma, Jumanne, tarehe 6 Machi 2018. Tume hii imekuwa mstari wa mbele kuhasisha uwajibikaji wa kuwapokea wahamiaji katika ngazi ya kimataifa kwa kuitisha majukwaa ya mikutano kimataifa kuhusu wahamiaji na maendeleo.

Matunda ya juhudi hizi ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa Wahamiaji, maarufu kama "Global Compact" changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuondokana na kisingizio cha usalama wa taifa, sera na mikakati ya kisiasa isiyopenda kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, ambao ni rasilimani inayopaswa kutumiwa vyema kwa kuheshimu haki zao, utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kardinali Parolin anasema, kuna haja ya kusoma alama za nyakati ili kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na wakimbizi pamoja na wahamiaji, ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine duniani!

Majadiliano katika ukweli na uwazi; katika mshikamano wa huduma na upendo, yatasaidia kuokoa maisha ya watoto, wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Watoto wanapaswa kulindwa, kuheshimuwa pamoja na kupatiwa huduma msingi za elimu, afya na maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani:  “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapoea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha!

Akizungumzia kuhusu mkakati huu wa kichungaji Kardinali Parolin anakiri kwamba, viongozi wengi wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa wanalipongeza Kanisa katika mchakato wa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Huu ni ushuhuda wa ari na moyo wa mshikamano wa kinabii unaofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kukuza na kudumisha Injili ya upendo na mshikamano; majadiliano ya kiekumene na kidini katika huduma makini kwa binadamu sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.