Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Ungama dhambi zako na wala si za jirani yako!

Papa Francisko anawataka waamini kukimbilia Kiti cha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili waweze kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.

06/03/2018 14:55

Kila mwamini anapaswa kuchunguza dhamiri yake mbele ya Mwenyezi Mungu katika kioo cha ukweli na uwazi, ili aweze kutubu na kumwongokea Mungu bila kuwashutumu wengine. Waamini wanaalikwa kukimbilia kwenye Mahakama ya Huruma ya Mungu, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa kutambua kwamba, wao ni wadhambi, lakini Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo. Waamini wakumbuke kwamba, dhambi inachafua uhusiano kati yao na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, kumbe, Sakramenti ya Upatanisho, imsaidie mwamini mmoja mmoja, kurejesha tena uhusiano mwema na Mungu pamoja na jirani zake, ili kuomba neema na wokovu!

Jambo la msingi ni waamini kujenga utamaduni wa kuwasamehe na kusahau, kama ambavyo Mwenyezi Mungu anawasamehe kila mara wanapokimbilia huruma na upendo wake wa milele! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 6 Machi 2018, wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Waamini kamwe wasijenge utamaduni wa kutaka kulipiza kisasi, kwa kutambua kwamba, kabla ya yote, Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwasamehe pale walipotumbukia dhambini.

Kiini cha Liturujia ya Neno la Mungu ni toba na msamaha kama anavyosimulia Nabii Danieli akimwomba Mwenyezi Mungu kutotangua agano lake wala kuwaondolea rehema zake, kwani wamekuwa duni kuliko mataifa mengine yote kwa sababu ya dhambi zao. Lakini kwa moyo uliovunjika na kupondeka pamoja na roho nyenyekevu wakubaliwe mbele yake, awatendee kadiri ya fadhili zake, sawa sawa na wingi wa huruma yake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, sala hii ni muhimu sana kwa waamini kuweza kupata msamaha wa dhambi zao mbele ya Mwenyezi Mungu.

Waamini wanapokwenda kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, waungame dhambi zao na wala si dhambi za wengine! Waoneshe moyo wa toba na wongofu wa ndani, daima wakipania kuachana na dhambi pamoja na nafasi zake, ili waweze kuhesabiwa haki mbele ya Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kusamehe na kusameheana kama ndugu, ili waweze pia kupata msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, daima wakioneshana huruma. Waamini wasikubali hata kidogo, kuwa watumwa wa Ibilisi kwa kumezwa na chuki na uhasama, bali watambue na kuguswa na huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwanzo wa maisha mapya! Wawe tayari kusamehe hata saba mara sabini kama ambavyo Kristo Yesu alimwambia Mtakatifu Petro kwa macho makavu kabisa bila hata kupepesa macho! Kwa njia hii, hata wao pia wataweza kupata msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

06/03/2018 14:55