2018-03-06 15:09:00

Papa Francisko: Uinjilishaji unafumbatwa katika huduma ya upendo!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa kongamano la Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko litakalofanyika mjini Roma, tarehe 10 Machi 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Uhusiano kati ya Upendo na Utamadunisho: Kituo cha Afya cha Sabou, Burkina Faso” anawataka kukuza na kudumisha mwingiliano huu kama njia ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa familia ya Mungu nchini Burkina Faso.

Baba Mtakatifu anasema, kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kujizatiti na kuzingatia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa unaojikita katika uinjilishaji na maendeleo endelevu ya binadamu! Anawaalika wajumbe wa mkutano huu, kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sala na sadaka zao. Kituo cha Afya cha Mtakatifu Marximilian Maria Kolbe kilichoko huko Sabaou, nchini Burkina Faso, kilianzishwa kunako mwaka 2003, ili kuchangia mchakato wa maboresho ya huduma ya afya kama sehemu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kipaumbele cha pekee ni huduma kwa mama na mtoto, ili kuweza kuokoa maisha ya watoto wengi ambao walikuwa wanakabiliwa na kifo hata kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano. Kongamano hili linahudhuriwa na Balozi Josephine Ouedraigo, Balozi wa Burkina Faso mjini Vatican, Bwana Nicolas Meda, Waziri wa Afya kutoka Burkina Faso pamoja na viongozi wakuu kutoka Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.