2018-03-06 14:30:00

Papa Francisko kwa Maaskofu wa Vietnam: Injilisheni kwa furaha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam linaloundwa na majimbo 26 limegawanywa katika majimbo makuu matatu ili kurahisisha huduma ya kichungaji kwa watu wa Mungu nchini Vietenam. Kuna zaidi ya Parokia 2, 200 zinazohudumiwa na Mapadre 400 wanaojisadaka kila siku ya maisha, ili kutekeleza dhamana na utume wao katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 18 Machi 2018 Maaskofu kutoka Vietnam wanafanya hija ya kitume, inayotekelezwa walau mara moja katika kipindi cha miaka mitano kwa kukutana na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 5 Machi 2018 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam kwa kuwataka kuendeleza dhamana ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha na furaha ya Injili, ili kuwashirikisha watu wa Mungu nchini Vietnam matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa kati pamoja na watu, kwa kuwasikiliza kwa makini na kuwahudumia kwa unyenyekevu na upendo mkuu.

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Askofu Joseph Dinh Duc Dao, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam anasema, katika mazungumzo yao na Baba Mtakatifu Francisko wamegusia changamoto, fursa na matatizo wanayokumbana nayo katika mchakato mzima wa uinjilishaji na ushuhuda wa Injili Barani Asia. Baba Mtakatifu ameonesha uwepo wake wa karibu kama Baba na ndugu kwa familia ya Mungu nchini Vietnam. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, dhamana na utume wa uinjilishaji nchini Vietnam unafumbatwa katika furaha ya Injili na matumaini yanayobubujika kwa namna ya pekee katika maisha ya sala na tafakari; ushuhuda na uwepo wa viongozi wa Kanisa kati pamoja na watu wao, lakini zaidi kwa wakleri wao ambao ni wasaidizi wao wa kwanza katika mchakato mzima wa uinjilishaji.

Waamini wengi nchini Vietnam wanapenda kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, licha ya changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia inavyoingia kwa kasi nchini Vietnam. Kutokana na changamoto hizi zote, Kanisa nchini Vietnam linapenda kujikita zaidi katika katekesi makini ya awali na endelevu, ili kuwasaidia waamini kufahamu misingi ya imani yao, tayari kuishuhudia. Ili kuweza kukabiliana na changamoto za elimu na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya, Kanisa nchini Vietnam linashauriwa na Vatican kuanzisha Chuo kikuu cha Kikatoliki, ingawa hii bado ni changamoto kubwa nchini humo. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki Vietnam kuwa na ujasiri, imani na matumaini; mambo yatakayowawezesha kuthubutu kutekeleza dhamana na wajibu wao pasi na woga wala makunyanzi! Kanisa lina matumaini makubwa kwa familia ya Mungu Barani Asia, licha ya changamoto za majadiliano ya kidini na kitamaduni; haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.