Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Kardinali Baldisseri: Sinodi ya Vijana 2018 ni moto wa kuotea mbali!

Utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ni sehemu ya mchakato wa Kanisa wa ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani. - AFP

06/03/2018 07:27

Kanisa linataka kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza, kuambatana na kuwasindikiza vijana ili kuweza kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazopatikana katika maisha yao. Kanisa linataka kushuhudia imani ya vijana, kusikiliza wasi wasi na mashaka wanayoyafumbata katika sakafu ya nyoyo zao! Kanisa linataka kusikiliza hata “mahangaiko” yanayowakera vijana katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo, ili kuboresha sera na mikakati ya utume kwa vijana. Ndiyo maana hitimisho la utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana litakuwa ni sehemu ya “Hati ya Kutendea Kazi” “Instrumentum Laboris” itakayowasilishwa kwa Mababa wa Sinodi, Mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican.

Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kuitisha utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, tukio litakalowashirikisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hasa katika maeneo yenye kinzani, vita na migogoro ili kuweza kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao, tayari kuibua mbinu mkakati utakaoliwezesha Kanisa kuwatangazia vijana Injili ya matumaini.   Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yatakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 19 - 24 Machi 2018. Kanisa linawataka vijana kuwa ni wadau wakuu katika maadhimisho ya Sinodi ya vijana. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni Sinodi itakayokuwa na uwakilishi mpana zaidi: kwa kuwajumuisha vijana wakristo na waamini kutoka katika dini mbali mbali duniani. Papa Francisko anataka kujenga utamaduni wa Kanisa kuwasikiliza vijana “mubashara” bila kizuizi, ili kuwajengea ari na moyo wa kujiamini na hatimaye, kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya matumaini katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Lorenzo Baldisseri akizungumzia kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, yatakayokuwa na utangulizi wake mwezi Machi, 2018 amefafanua vipaumbele kwamba: Kwanza kabisa ni kuwajengea uwezo vijana ili kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Vijana. Hii ni Sinodi ya vijana kwa ajili ya vijana pamoja na vijana. Jambo la msingi ni mchakato wa ujenzi wa ”Utamaduni wa Kusikiliza Vijana” dhana inayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko, ili kuwafahamu vijana: matatizo, changamoto na fursa walizo nazo katika maisha, ili waweze kutekeleza vyema dhamana, wito na majukumu yao katika mwanga wa Injili ya Kristo, Kanuni maadili na utu wema!

Kanisa linataka kuwasikiliza vijana wanaotoka pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya jamii, ili kusikiliza matamanio yao halali, ili hatimaye, Kanisa liweze kufanyia kazi! Hii ni hatua muhimu kuelekea katika maadhimisho ya Sinodi ya vijana ambayo ni hatua itakayowaunganisha vijana na Mababa wa Kanisa, ili kuibua mbinu mkakati wa utume kwa vijana daima Kanisa likijitahidi kusoma alama za nyakati! Utangulizi wa Sinodi ya vijana utawashirikisha: wawakilishi wa wazazi, walezi, waalimu, wakleri, watawa na baadhi ya wadau wa utume wa vijana sehemu mbali mbali za dunia. Huu utakuwa ni muda wa kubadilishana mang’amuzi, uzoefu na mikakati mbali mbali ya utume kwa vijana. Ni nafasi ya watu kutoka katika tamaduni, mila na desturi mbali mbali kukutana ili kujadiliana ili kupembua kwa kina na mapana: maisha ya ujana, imani, kanuni maadili na utu wema na jinsi ambavyo Kanisa linaweza kujibu changamoto hizi katika ukweli na uwazi kwa kuzingatia tunu msingi za Kiinjili. Lengo ni kuwawezesha vijana kutambua thamani ya maisha kila kijana kadiri ya wito katika maisha yake.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anakaza kusema, yale yote yatakayojadiliwa katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi na hatimaye, kutolewa ushauri na mapendekezo ya vijana wa kizazi kipya, yatawasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 25 Machi 2018, Jumapili ya Matawi ambayo pia ni Siku ya Vijana Kijimbo! Hii ni siku ambayo inatarajiwa kuwashirikisha vijana wengi zaidi kwa njia ya mitandao ya kijamii kama jukwaa jipya la kuwakutanisha vijana, ili kutoa maoni na ushauri wao utakaozingatiwa katika mchakato mzima wa kuandika ”Hati ya Kutendea Kazi” kwa ajili ya Sinodi ya Vijana. Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu inayoongoza Siku ya XXXIII ya Vijana Duniani ni ”Usiogope Maria, kwa maana umepata neema kwa Mungu”. Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kukutana na uwakilishi mkubwa wa vijana ili kuadhimisha kwa pamoja Siku ya Vijana Kijimbo.

Kwa upande wake, Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu anasema, kumekuwepo na ushiriki mkubwa wa vijana kati ya umri wa miaka 16- 19 katika kujibu maswali dodoso yaliyoandaliwa kama sehemu ya ”Hati ya ya Maandalizi ya Sinodi”. Vijana wengi wameguswa kuhusu mada ya umuhimu wa dini katika maisha. Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanatakiwa kuwa na uwakilishi mkubwa wa vijana watakaokuwa ni sauti ya vijana wenzao hasa katika: malezi seminarini na katika nyumba za kitawa; wawakilishi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu; wasanii na wachezaji; watu wa kujitolea na vijana walioko kwenye masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi, bila kuwasahau wawakilishi wa vijana kutoka katika madhehebu na dini mbali mbali katika maeneo yao. Wawakilishi wa vijana kutoka magerezani, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na walemavu.

Kijana Marilene Nishimwe kutoka Burundi aliyeshiriki katika mkutano wa kuwasilisha yale yatakayojiri kwenye maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya vijana anasema, katika maadhimisho ya Sinodi ya Vijana 2018, vijana wanaweza kushirikishana mawazo kwa njia ya mitandao ya kijamii ili kuwaunganisha vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vijana wanaweza kuperuzi katika mtandao wa Sinodi ya Vijana kwa anuani ifuatayo: www.synod2018.va . Hapa vijana wataweza kupata maelezo ya jinsi ya kujiunga katika makundi mbali mbali ya mitandao ya kijamii kama vile ”Facebook” ambayo iko katika lugha sita! Wanaweza kutumia pia Hashtag #Syno2018 na Instagram pamoja na mitandao mingine ya kijamii. Ama kwa hakika, Sinodi ya vijana ni moto wa kuotea mbali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

06/03/2018 07:27