2018-03-05 08:00:00

Watoto wakimbizi na wahamiaji kuwekwa vizuizini kuna madhara makubwa


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018 alijikita kwa namna ya pekee katika mantiki ya “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati! Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaobisha hodi kwenye malango ya watu sehemu mbali mbali duniani, ni nafasi muhimu sana ya kuweza kukutana na Kristo Yesu, ambaye anajitambulisha kama mkimbizi na mhamiaji anayekataliwa na kubezwa na watu wa nyakati mbali mbali.

Mama Kanisa anapenda kuwaonesha upendo wake wa dhati, wakimbizi na wahamiaji, katika hatua mbali mbali za safari yao, tangu wanapoondoka, wanapofika na hatimaye, kurejea tena makwao hali inaporuhusu. Waamini wakishirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kuyavalia njuga matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwaonesha moyo wa ukarimu, hekima na busara kila mmoja kadiri ya uwezo na nafasi yake. Lakini, wote kwa pamoja wanaweza kujibu changamoto hizi kwa kujikita katika mchakato unaofumbatwa katika mambo makuu yafuatayo: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji”.

Monsinyo Michael Czerny, Katibu mkuu Msaidizi, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, Idara ya Wakimbizi na wahamiaji, anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti zaidi ili kuhakikisha kwamba: watoto wakimbizi na wahamiaji; utu na heshima yao vinalindwa na kudumishwa; haki zao msingi zinapatikana na kuendelezwa pamoja na kupatiwa huduma ya maendeleo endelevu ili kuwajengea leo na kesho yenye matumaini zaidi. Changamoto hii haina budi kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wanaojikuta wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za uso wa dunia.

Kipaumbele cha kwanza ni kuwalinda watoto hawa kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Watoto hawa walindwe na kuheshimiwa utu wao; wapewe mahitaji yao msingi kama vile: huduma bora ya afya na elimu pamoja na kuunganishwa tena na wazazi na walezi wao, kwa ajili ya ustawi wa familia nzima pamoja na makuzi yao yanayozingatia maendeleo endelevu ya binadamu. Vatican inapenda kuihamasisha Jumuiya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti kikamilifu kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa wakimbizi na wahamiaji, lakini zaidi, kwa kuwahudumia watoto ambao wametengana na wazazi pamoja na familia zao.

Jambo la kwanza linalopaswa kuangaliwa kwa makini ni kukomesha vitendo vya kuwaweka watoto wakimbizi na wahamiaji vizuizini, kwani madhara yake ni makubwa sana kwa ukuaji na ukomavu wa watoto hawa ambao wanateseka kama wakimbizi na wahamiaji. Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres imeyabainishwa hayo. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa ni kutoa njia mbadala ya watoto wakimbizi na wahamiaji ili wasitumbukizwe vizuizini.

Hii inawezekana ikiwa kama kutakuwepo na njia za kisheria zitakazosaidia kuwaunganisha tena watoto pamoja na familia. Pili ni kuandaa uwezekano wa watoto kuishi pamoja na wazazi na walezi wao. Tatu ni kuwapatia watoto hawa ambao wanatambuliwa kisheria kuwa ni wale wenye umri chini ya miaka 18 nafasi ya kuendelea na masomo pamoja na kupata fursa za ajira. Kimsingi, Mkataba wa Kimataifa juu ya usalama wa Wahamiaji, maarufu kama "Global Compact" ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuondokana na kisingizio cha usalama wa taifa, sera na mikakati ya kisiasa isiyopenda kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, ambao ni rasilimani inayopaswa kutumiwa vyema kwa kuheshimu haki zao, utu na heshima yao kama binadamu!

Baba Mtakatifu anapenda kuialika Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, pamoja na kuzingatia usalama wa taifa, lakini pia wanapaswa kimaadili kuwapokea na kuwakirimia watoto wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na ustawi wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.