Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Majadiliano ya kiekumene

Uekumene wa huduma kama ushuhuda wenye mvuto katika uinjilishaji

Makanisa Barani Afrika yanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Upendo inayomwilishwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. - AP

05/03/2018 10:27

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Uinjilishaji Ulimwenguni, utakaofanyika Jijini Arusha, Tanzania, kuanzia tarehe 8-13 Machi 2018; kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika Roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”. Huu ni mkutano unaoyashirikisha kwa namna ya pekee kabisa, Makanisa Barani Afrika, kama wenyeji wa mkutano huu wa kimataifa, unaofanyika wakati huu ambako kuna changamoto kubwa ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mkutano huu ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Padre Richard Nnyombi kutoka Shirika la Wamisionari wa Afrika ambaye amebahatika kutekeleza utume wake wa kimisionari nchini Algeria, Tanzania, Kenya, Uganda na Italia kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huu, anakazia zaidi kuhusu mchango wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika mchakato mzima wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa kwa namna ya pekee katika: uekumene wa damu ambao kimsingi ni ushuhuda wa maisha na tunu msingi za Kikristo ambao unapelekea hata mwamini kumwaga damu yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Ni uekumene wa sala na maisha ya kiroho yanayopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa uinjilishaji. Uekumene wa huduma unajikita katika Injili ya huruma na mapendo ya Mungu, kielelezo cha imani tendaji.

Kanisa Katoliki katika kipindi cha miaka 50 tangu baada ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican limepiga hatua kubwa katika mchakato mzima wa majadiliano ya kiekumene yanayoendelea kufafanuliwa katika nyaraka, matamko na maadhimisho mbali mbali kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa mbali mbali ya Kikristo, kwa kutambua kwamba, utume wao wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo unapata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa njia hii, Wakristo wanashiriki kikamilifu katika utume wa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Lengo ni kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Changamoto ya kwanza kwa wakati huu ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwa njia hii, binadamu ataweza kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na kuendeleza mazingira kama sehemu ya kazi ya uumbaji. Uinjilishaji unapaswa kuwasukuma Wakristo kwenda pembezoni mwa jamii ambako kuna maelfu ya watu wanaoteseka kutokana na vita, njaa, umaskini, magonjwa na ujinga; mambo ambayo yanafifisha utu na heshima ya binadamu.

Kanisa Katoliki linakazia pia umuhimu wa ushiriki mkamilifu katika maisha ya Kisakramenti kama njia ya kujipatia neema, baraka na nguvu ya kusonga mbele katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mataifa. Maskini na wanyonge ni watu waliopata upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani. Hata leo hii, kuna watu ambao bado wanaendelea kuathirika kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu, kiasi kwamba, utu na heshima yao vinawekwa rehani kutokana na ubinafsi, uchoyo, uchu wa mali na madaraka. Watu wanasukumizwa pembezoni katika masuala ya kisiasa na kijamii; kitamaduni na kiuchumi; kiutu na kimaadili; kiroho na katika maisha ya kidini. Maskini na wanyonge wanapaswa kuwezeshwa kwa kujengewa uwezo wa kimaadili, kiutu, kijamii, kisiasa na kiroho ili kuweza kupambana na hali pamoja na mazingira yao, kwa njia ya amani inayofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Padre Richard Nnyombi anasema, ili kufikia lengo hili kuna haja ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekimene na kidini; kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama kielelezo cha imani tendaji. Wakristo washikamane pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ekolojia dhidi ya uharibifu na uchafuzi wa mazingira ambao kwa sasa ni chanzo kikuu cha maafa na umaskini unaowasibu watu wengi duniani. Umoja na mshikamano kati ya Makanisa tajiri na yale yaliyoko katika nchi za kimisionari ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa na ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma ni muhimu sana kama kielelezo makini cha uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Watu wengi wanaguswa kwa vitendo na wala si kwa maneno matupu ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa kama wanavyosema waswahili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

05/03/2018 10:27