2018-03-05 07:46:00

Papa Francisko: Safisheni mahekalu ya miili yenu yasiwe pango la wevi


Liturujia ya Neno la Mungu kadiri ya Mwinjili Yohane inamwonesha jinsi Kristo Yesu, alivyowafakuza wafanyabiashara kutoka katika Hekaluni kwani walikuwa wameligeuza kuwa ni nyumba ya biashara. Hili ni tukio ambalo Yesu alilifanya wakati Siku kuu ya Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa inakaribia, kiasi kwamba, liliacha mshangao mkubwa miongoni mwa watu pamoja na uadui kwa wakuu wa Makuhani na wale wote waliokuwa wameguswa katika shughuli zao za kiuchumi.

Tukio hili lilitafsiriwa kama ushuhuda wa kinabii, ambao daima ulitolewa na Manabii kwa niaba ya Mwenyezi Mungu, kwa kulaani vitendo vyote vilivyokuwa vinadhalilisha Hekalu Takatifu, ndiyo maana hakukuwepo na ghasia wala vurugu kiasi cha Polisi wa kutuliza ghasia kuingilia kati! Hii ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe 4 Machi 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wayahudi walimuuliza Yesu ni kwa mamlaka gani alikuwa anatenda yote haya?

Lakini wakasahau kwamba, alikuwa anatenda kwa jina la Mwenyezi Mungu, kama Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kristo Yesu, alikuwa amepania kulitakatifuza Hekali la Mungu, ndiyo maana baada ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake, wanafunzi wakayakumbuka maneno yake kwamba, ilikuwa imeandikwa katika Zaburi ya 69 kwamba, “Wivu wa nyumba yako utanila”. Ni sala ya kuomba msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika hali tete ya maisha kutokana na uadui uliojengeka, utakaofikia kilele chake katika mateso na kifo chake Msalabani.

Wivu wa nyumba ya Baba yake, ilikuwa ni hamu ya kutekeleza upendo wa hali ya juu, uliokuwa umefumbatwa katika sadaka, kwa Kristo Yesu, kujitoa mwenyewe, ili kumtii na kumtumikia Baba yake wa mbinguni katika ghasia na vurugu kama hizi. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, ushuhuda wa mamlaka ya Kristo Yesu utakuwa ni mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu. Ndiyo maana akawaambia wakuu wa Makuhani, bomoeni Hekalu hili nami nitalijenga kwa muda wa siku tatu! Mwinjili Yohane anakaza kusema, Kristo Yesu alikuwa anazungumzia kuhusu Hekalu la Fumbo la Mwili wake. Pasaka ya Kristo Yesu, ikafungua ibada mpya, inayoadhimishwa katika Hekalu jipya ambalo ni Kristo mwenyewe kwa njia ya upendo mkamilifu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanaishi hapa duniani si kwa kutafuta mafao na masilahi yao binafsi, bali yote yawe ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu ambao ni upendo wake usiokuwa na mipaka. Wanakumbushwa kwamba, kamwe wasiifanye miili yao kuwa ni soko! Na kwa namna ya pekee kabisa, kamwe Kanisa lisigeuzwe kuwa soko la mambo ya kidunia, kwa kuendelea siku kwa siku kutafuta masilahi ya mtu binafsi, badala ya kujikita katika upendo wenye ukarimu na mshikamano. Mafundisho haya ya Kristo Yesu, si tu yanaelekezwa kwa Jumuiya Kikanisa, bali hata kwa watu binafsi, jumuiya mbali mbali na jamii katika ujumla wake. Kwa kawaida, kuna kishawishi cha kutaka kutumia mamlaka kwa ajili ya mambo binafsi na wakati mwingine yanayokwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu. Kuna baadhi ya watu wanamtumia Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao yao binafsi, ndiyo maana Kristo Yesu, ameamua kutoa fundisho hili kwa ukali zaidi. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko, anamwomba Bikira Maria, awasaidie waamini katika kipindi hiki cha Kwaresima, kumtambua Mwenyezi Mungu kama Bwana na mwokozi wao, ili kusafisha kutoka nyoyoni na katika matendo yao kila aina ya kufuru kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.