Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko anawaonya waamini kutochezea imani!

Papa Francisko anawataka waamini kutubu na kuongoka ili waweze kufikiri na kutenda kadiri ya mwanga wa Roho Mtakatifu na kamwe wasichezee imani!

05/03/2018 11:37

Naamani, jemadari wa Jeshi la Mfalme wa Shamu aliponywa ukoma wake kama inavyosimuliwa kutoka kwenye Kitabu cha Pili cha Wafalme. Kwa upande mwingine, Mwinjili Luka anamwonesha Kristo Yesu akikataliwa mjini Nazareti. Yesu anachukua fursa hii kuwakumbusha wasikilizaji wake kwamba, hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake Jumatatu, 5 Machi 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilicho mjini Vatican ameonya kwamba, Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Kwaresima, anawataka watoto wake kufanya toba na wongofu wa mawazo mintarafu mafundisho ya Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu anaonya kwa mara nyingine tena kwamba, ni hatari sana kwa waamini kuchezea dini na imani, kumbe wanahitaji kutubu, kuongoka katika mawazo, maneno na matendo yao! Mama Kanisa katika kipindi cha Kwaresima anatoa dawa ya maisha ya kiroho inayofumbatwa katika: kufunga na kusali; kufanya matendo ya huruma na mapendo pamoja na kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili liweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao ya Kikristo! Mfano wa Msamaria mwema uwe ni kielelezo cha huduma ya upendo na mshikamano kwa Wakristo wote, ili kufikiri na kutenda kadiri ya mafundisho ya Kristo Yesu na wala si vinginevyo!

Baba Mtakatifu anasema Naamani, jemadari wa Jeshi la Mfalme wa Shamu alikuwa shujaa lakini alikuwa na ugonjwa wa ukoma. Akashauriwa na Elisha Mtumishi wa Mungu kwenda kuoga katika Mto Yordani mara saba, lakini Naamani akakasirika na kuondoka, kwani alidhani kwamba Elisha angetoka na kuja mbele yake ili kumwombea  ili aweze kumpona. Naamani alitarajia Mwenyezi Mungu amfanyie muujiza ambao ungewashtua wengi na kusahau kwamba, Mwenyezi Mungu anatenda kadiri anavyotaka. Roho Mtakatifu anatenda katika nyoyo za watu kadiri anavyotaka ndiyo maana Kristo Yesu aliporudi kwa nguvu ya Roho, akaenda Galilaya, naye alikuwa akifundisha katika Masinagogi yao, akitukuzwa na watu wote.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika “Msafara wa Mamba, kenge hawakosekani hata kidogo!” Baadhi ya watu wakaanza kusema, “Huyu siye Mwana wa Yusufu?” Walitaka Yesu afanye miujiza kama alivyofanya sehemu nyingine, lakini hakufanya muujiza wowote kwani ni Roho Mtakatifu na Neno la Mungu ndilo linalotenda kazi katika nyoyo za watu! Kamwe watu wasichezee imani! Maisha ya Mkristo yanapaswa kufuata nyayo za Kristo Yesu, vinginevyo ni ubatili mtupu! Waamini wawe na ujasiri wa kufanya toba na wongofu wa mawazo ili kuondokana na kufikiri na kutenda kwa mazoea. Wakristo wafikiri na kutenda mintarafu mwanga wa Injili, wawe na ujasiri wa kuomba neema ya toba na wongofu wa kufikiri na kutenda kama Kristo Yesu alivyofundisha katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho yake makuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

05/03/2018 11:37