Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Majadiliano ya kiekumene

Askofu Mkuu Fredrick Shoo: Arusha kumekucha! Mkutano wa Uinjilishaji!

Askofu Fredrick Shoo anawakaribisha wajumbe wa mkutano mkuu wa uinjilishaji ulimwenguni unaofanyika Jijini Arusha nchini Tanzania kuanzia tarehe 8 - 13 Machi 2018. - REUTERS

05/03/2018 07:30

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kukamilisha maandalizi kwa ajili ya maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Uinjilishaji Ulimwenguni, utakaofanyika kwenye kilima cha Ngurdoto, Arusha, Tanzania, kuanzia tarehe 8 -13 Machi 2018; kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika Roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”. Wajumbe 800 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huu. Askofu Mkuu Fredrick Shoo wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, Dayosisi ya Arusha anasema, huu ni mkutano utakaoyashirikisha kwa namna ya pekee kabisa, Makanisa Barani Afrika, kama wenyeji wa mkutano huu wa kimataifa, unaofanyika wakati huu ambako kuna changamoto kubwa ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu Mkuu Fredrick Shoo anasema, ni matumaini yake makubwa kwamba, wajumbe watapata muda wa kuabudu, kutafakari na kuchangia hoja zao kama sehemu ya maadhimisho ya utume ambao Mwenyezi Mungu amelikabidhi Kanisa lake, hasa wakati huu, watu wanapoendelea kukengeuka na kumwasi Mungu; wanapojikuta wakivunjilia mbali Amri na Maagizo ya Mwenyezi Mungu; wanapojikuta wakibobea katika uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote! Ni wakati wa kusimama na kutafakari kuhusu umuhimu wa jamii kujikita katika haki msingi za binadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na maridhiano. Wakati huu wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kuna haja kwa Wakristo kutafakari kwa kina na mapana umuhimu wa tasaufi katika maisha ya mwanadamu na jinsi ambavyo kama wafuasi wa Kristo Yesu wanavyoitwa kukabiliana na changamoto hii.

Askofu Mkuu Fredrick Shoo anasema, mkutano huu utajikita katika mambo makuu manne: utume wa Makanisa ulimwenguni, majadiliano ya kiekumene; Makanisa Barani Afrika na utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Baraza la Makanisa Ulimwenguni limewataka wajumbe kujizatiti kikamilifu katika kukabiliana na changamoto hizi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kutoa majibu muafaka, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuongoza historia na maisha ya mwanadamu, hadi pale kazi ya uumbaji na ukombozi itakapofikia utimilifu wake. Mada hizi zinahitaji ari na moyo mkuu kuweza kuzijadili kwa kina na mapana na hatimaye, kuibua mbinu mkakati utakaovaliwa njuga na Makanisa ndani nan je ya Bara la Afrika, ili kupambana fika na utamaduni wa kifo unaotishia Injili ya uhai!

Askofu Mkuu Fredrick Shoo anaendelea kufafanua kwamba, Wakristo wanapaswa kuwa ni wafuasi wanaobadilika kwa kusoma alama za nyakati, tayari kuubeba Msalaba wao na kuanza kufuata nyayo za Kristo Yesu. Woga na ubinafsi ni vikwazo vikuu katika mchakato mzima wa mabadiliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu ambaye ni Bwana wa Msalaba, Ufufuko na Uzima anawafundisha wafuasi wake  kwa kuwataka kujikana wenyewe, kuubeba Msalaba wao na kumfuasa kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu kwa ajili ya Injili. Askofu MkuuFredrick Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania anasema, kumekuwepo na ushirikiano mkubwa wakati wote wa maandalizi ya mkutano huu kati ya Kanisa la Kiilnjili la Kiluteri Tanzania na Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Familia ya Mungu nchini Tanzania inapenda kuwakaribisha Mababa wa Kanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwenda Tanzania ili kujionea utajiri wa maliasili; kuonja ukarimu na wema wa watanzania sanjari na kujifunza mambo mema na mazuri kutoka kwa watanzania!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

05/03/2018 07:30