Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Hekalu ni Fumbo la Mwili wa Kristo, kielelezo cha uwepo wa Mungu!

Hekalu ni mahali patakatifu ambapo mwamini anakutana na Mwenyezi Mungu katika maisha pamoja na kuonja utukufu na uwepo wake wa daima kati ya watu wake. - AP

03/03/2018 08:30

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News! Siku arobaini za kipindi cha Kwaresima ni siku zinazotusaidia kujiunda upya, yaani kufanya marekebisho yanayotupasa ili maisha yetu  yazidi kuuelekea ule mpango wa Mungu wa kutuleta duniani na mpango wake mzima wa kutukomboa.  Njia hii ya kujiunda upya si njia isiyo na vikwazo, kutoka ndani yetu sisi wenyewe lakini pia kutoka katika mazingira tuliyomo. Tunaalikwa kumpa Kristo nafasi ya kwanza katika safari yetu hii. Yeye  aliye Njia, Ukweli na Uzima atatuongoza vema kuifikia Pasaka ya milele yalipo makusudio yetu sisi waamini wake.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Kut. 20:1-7) linahusu amri kumi ambazo Mungu aliwapa waisraeli katika Mlima Sinai walipokuwa wakitoka utumwani Misri kuelekea nchi ya ahadi Kanaani. Kwa kuwapa amri hizi, Mungu alitaka kuwaunda kama taifa na kuweka nao Agano kwamba watakuwa watu wake na yeye atakuwa Mungu wao. Tunaweza kusema ni kwa njia ya agano hili ndio walianza kutambuliwa kama taifa la israeli kwani hapo awali walikuwa ni kama ukoo au kabila tu la Waebrania. Maisha yao yote yaliyofuata baada ya hapa yalipimwa daima katika mzani wa amri hizi kumi, kwa namna walivyozishika au kwa namna walivyozipuuzia.

Amri hizi zinaeleza maisha wanayopaswa kuishi sasa kama watu wa Mungu wanapoingia nchi ya ahadi. Sehemu yake ya kwanza, yaani amri ya kwanza hadi ya tatu ni kuhusu mahusiano yao na Mungu na sehemu yake ya pili, yaani amri ya nne hadi ya kumi ni kuhusu mahusiano yao wao kwa wao. Mgawanyo huu pia unasisitiza uhalisia kuwa maisha yao na mahusiano kati ya wao kwa wao (amri ya 4 hadi ya 10) yanapaswa kuongozwa na kadiri atakavyo Mungu (amri ya 1 hadi ya 3).

Somo la pili (1Kor. 1:22 - 25) ni mafundisho ya Mtume Paulo juu ya namna mazingira ya mahali yanavyoweza kuwa kikwazo kwa kuzipokea kweli za kimungu na kweli za kiimani. Katika Korinto,  kipindi alichohubiri Mtume Paulo kilikuwa ni kipindi cha ugunduzi mkubwa wa elimu ya falsafa na hoja. Kila aliyekuwa akifundisha alikuwa akijipanga kwa hoja za kifalsafa na ujuzi wa kucheza na maneno ili kuwashawishi wasikilizaji. na kwa sehemu kubwa umahiri wa mwalimu na uwezo wake wa kushawishi vilipewa thamani kubwa kuliko ujumbe wenyewe. Kumbe mafundisho yoyote ambayo hayakuzingatia mfumo huo wa hoja na uchezaji wa maneno yalionekana kuwa ni upuuzi tu. Paulo alipokwenda kuhubiri kwao Habari Njema hakuenenda kadiri ya waalimu wao bali juu ya ujumbe wa Kifo cha Kristo kilicholeta ukombozi kwa ulimwengu mzima. Hapo waliona ni upuuzi tu.

Mafundisho haya kuhusu Kifo cha Kristo kilicholeta wokovu, kwa wayahudi ambao hawakuwa wameongokea ukristo yalionekana kuwa ni kikwazo. Hii kwa sababu kwa mila zao mtu aliyekufa kwa kutundikwa msalabani hakuwa na thamani na alionekana amelaaniwa. Sasa wangewezaje kumwamini huyo aliyekufa msalabani na kuamini kuwa kwa njia yake tu ndio wanaweza kuokolewa? Kwao kilikuwa ni kikwazo. Jibu na fundisho analolitoa Mtume Paulo kwa hali hii ni kwamba kuyaweka mafundisho ya Kristo katika mizani ya ubinadamu wetu kama kigezo pekee cha kuyapokea au kutokuyapokea ni kufanya makosa makubwa. Ni kujiwekea kizuio sisi wenyewe cha kuguswa na kukombolewa.

Somo la Injili (Yoh. 2:13-25) linaonesha Yesu analisafisha hekalu.  kadiri ya taratibu za kiibada za kiyahudi, wanyama walihitajika hekaluni ili kutolea dhabihu. Hali kadhalika wayahudi walipaswa kulipa zaka na zaka hii haikutolewa kwa fedha ya kigeni (ya Kaisari) kumbe, waliohitaji kulipa iliwabidi kubadilisha fedha. Kilichokuwa kinafanyika Hekaluni hapo ni kuwasubiri waliokuwa wanakuja kwa siku kuu na kuwauzia wanyama ili watolee dhabihu na pia kuwabadilishia fedha ili walipe zaka. Haya yote kwa yenyewe huenda yasingekuwa na shida. Shida inakuja pale ambapo vitendo hivi vya kibiashara vinachukua nafasi ya ibada yenyewe na tena vinawazuia wale wanaotaka kufanya ibada hekaluni wasiweze kufanya kwa sababu biashara hizi zinafanyika ndani ya hekalu lenyewe.

Hekalu la Mungu badala ya kuwa mahala pa watu kukutana na Mungu linakuwa ni mahala pa biashara hata bila kutaja uhalifu, unyang’anyi na wizi unaokuwa uanaambatana na biashara hizo. Hii ndiyo sababu Yesu anakasirika na anawafukuza wote waliogeuza nyumba ya Mungu kuwa nyumba ya biashara. Tendo hili pia ni tendo la kiishara kuwa Mwili wa Kristo ndio Hekalu hai. Litabomolewa (kifo chake Msalabani) lakini baada ya siku tatu atalijenga upya (Ufufuko). Mwili wa Kristo ndio hekalu hai lililotukuka ambalo kila aendaye kwake na kwa njia yake anao uhakika wa kukutana na Mungu.

Tafakari: Masomo haya katika kipindi hiki cha Kwaresma yanaleta kwetu mwaliko wa kujiunda upya, kujisafisha; kujitakasa. Ishara aliyoionesha Kristo kuwa mwili wake ndio hekalu hai ambalo kila aendaye kwake na kwa njia yake anapata uhakika wa kukutana na Mungu ni ishara anayotushirikisha pia na sisi kwa njia ya ubatizo. Kwa njia ya ubatizo mwili wa mkristo unafanyika kuwa hekalu la Roho Mtakatifu. Mwaliko wa leo wa kujiunda upya ni mwaliko wa kulisafisha hekalu hili kama Kristo alivyofanya. Yaani kuondoa yale yote yanayozuia nafsi kukutakana na Mungu. Ni mwaliko wa kusafisha mawazo yetu, maneno yetu, matendo yetu, vipaumbele vyetu, nia zetu na mengine mengi kama hayo. Lakini pia ni mwaliko wa kusafisha mazingira tuliyomo; tunayoishi na tunayofanyia kazi ili nayo yasiwe kikwazo kwetu kukutana na Mungu.

Mafundisho ya Mtume Paulo tuliyoyasikia katika somo la pili tayari yanatupa angalizo juu ya namna mazingira yanavyoweza kuwa kikwazo kupokea ujumbe wa Mungu na kufanya mabadiliko ndani yetu. Kwa Wakorintho mazingira yao yalikuwa ni ya elimu ya falsafa na kwa jinsi hiyo wakajikuta wanaupima ujumbe wa Mungu katika mazingira hayo kama kigezo cha kuupokea au la. Na tena si kwamba elimu hiyo ya falsafa iwasaidie kuupokea ujumbe wa Mungu bali ni kwamba ujumbe huo uendane kwanza na elimu yao ndio upokelewe.

Je, hii si kasumba yetu hata sisi? Kwamba, imani na matakwa yake yote yaingie kwanza katika vigezo vyetu na mifumo yetu ya maisha badala ya sisi kuingia katika matakwa yake? Mwaliko wa kujiunda upya ni mwaliko wa kukishinda kishawishi hiki na kutambua kuwa sio sisi tulio vigezo bali Mungu ndiye kigezo na tena anapaswa kuchukua nafasi ya kwanza. Kumpa Mungu nafasi ya kwanza ndio kukubali kuongozwa na amri zake alizotupatia.  Neema za kipindi hiki cha Kwaresima; mazoezi ya kiroho tufanyayo kwa njia ya kufunga, toba, sala na kuwasaidia wahitaji yatuzidishie nguvu ya kujiunda upya katika safari yetu ya imani, matumaini na mapendo!

Padre  William Bahitwa.

VATICAN NEWS.

03/03/2018 08:30