Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Jubilei ya Miaka 70 katika huduma!

Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa mwaka 2018 linaadhimisha Jubilei ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. - AFP

03/03/2018 09:31

Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika kipindi cha Mwaka 2018 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1948, likiwa na Makanisa wanachama 147 na tangu wakati huo zaidi ya Makanisa 200 yamejiunga na kuwa ni sehemu ya Baraza hili. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki ni mjumbe mtazamaji wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Baraza limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha umoja wa Makanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili Makanisa yote haya siku moja yote yawe na umoja chini ya Kristo Mchungaji mkuu.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeendelea kuratibu na kusimamia majadiliano ya kitaalimungu miongoni mwa Makanisa na matunda ya majadiliano haya yanaanza kuonekana. Kumekuwepo na maridhiano pamoja na matamko ya pamoja kuhusu: Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi; Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Dhamana na Utume wa Kanisa kama chombo na shuhuda wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili walimwengu waweze kumwamini Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa mstari wa mbele kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baraza litaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Baraza limeendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini kwa kuwashirikisha viongozi wa dini na Makanisa mbali mbali duniani, lakini zaidi kwa kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na mshikamano kati ya watu wa Mataifa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa ni jukwaa makini la kushirikishana: utajiri, amana na tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu. Limeendelea kudumisha mapokeo ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo  sanjari na kudumisha uekumene wa maisha ya kiroho; uekumene wa damu, uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Baraza limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Tangu mwaka 1992, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeragibisha haki ya mazingira kwa kutambua kwamba uchafuzi wa mazingira una maadhara makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika kipindi cha miaka 70 ya uwepo na utume wake, limekuwa mstari wa mbele kupambana na “ndago” za ubaguzi wa rangi, nyanyaso na dhuluma mambo ambayo yanatia kichefuchefu katika mchakato wa kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baraza pia limekuwa ni chombo cha huduma makini kwa watoto sehemu mbali mbali za dunia kwa: kwa kusimamia haki zao msingi, utu na heshima yao. Zaidi ya Makanisa mia moja, yanaendelea kutekeleza dhamana na wajibu huu wa kimaadili miongoni mwa watoto wadogo, lakini hasa wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Baraza la Makanisa kati ya mwaka 1976 hadi mwaka 1992 lilianzisha ofisi ya haki msingi za binadamu kwa ajili ya Amerika ya Kusini ambayo kwa wakati huo ilikuwa inatawalia kwa mabavu. Makanisa yakashikamana na kujifunga kibwebwe ili kuwasaidia waathirika wa tawala hizi za mabavu kupata haki zao msingi. Baraza la Makanisa Ulimwenguni likawa ni chachu ya huduma makini na rejea kwa maskini huko Amerika ya Kusini.

Kumbe, Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni fursa ya kuendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Makanisa; utekelezaji wa utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kujizatiti katika kujenga na kudumisha misingi ya haki  na amani, kama kikolezo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa hapo tarehe 21 Juni 2018 kutembelea Makao Makuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni huko Geneva, Uswiss. Kuanzia tarehe 8 hadi 13 Machi 2018, wajumbe zaidi ya 800 kutoka Makanisa mbali mbali duniani wanashiriki katika Mkutano mkuu wa Uinjilishaji Ulimwenguni,  kwenye kilima cha Ngurdoto, Jijini Arusha, Tanzania, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika Roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

03/03/2018 09:31