2018-03-02 11:11:00

Mapadre ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha; ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbali mbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!

Huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee, katika maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa wagonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kutoa mkazo wa pekee katika Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha.  Mapadre wanakumbushwa kwamba, utume wao wa Kipadre unajikita katika Sakramenti ya Upatanisho inayopaswa kufumbatwa katika ukarimu, ushuhuda, huruma; ukweli na uwazi katika kanuni maadili.

Mapadre wawe tayari kuwasindikiza waamini katika hija ya toba na wongofu wa ndani, kwa kuonesha uvumilivu; kwa kuwa na mawazo mapana na wakarimu katika kutoa msamaha wa Mungu. Mapadre pia wanapaswa kuwa ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani na kwamba, Sakramenti ya Upatanisho inapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya Kikristo kwani Mapadre ni vyombo vya Upatanisho. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume katika barua yake ya mwaliko kwa mapadre na mashemasi wanaotarajiwa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre hivi karibuni anawakumbusha kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni kiini cha maisha na utume wa Mapadre.

Kuanzia tarehe 5 – 9 Machi 2018, Idara imeandaa mafunzo ya ndani yatakayohitimishwa kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 9 Machi 2018 na baadaye jioni ataadhimisha Ibada ya Toba kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 11:00 jioni kwa saa za Ulaya! Kutakuwa na maungamo ya jumla na maondoleo ya dhambi yatakayotolewa kwa mwamini mmoja mmoja atakayejihimu kujongea katika Mahakama ya huruma ya Mungu, yaani “Kiti cha Kitubio”. Tayari idadi kubwa ya mapadre waungamishaji imekwisha kuandaliwa ili kutekeleza dhamana hii. Mafunzo haya yanagusia mambo msingi katika Sakramenti ya Upatanisho.

Monsinyo Krzysztof Józef Nykiel, Hakimu wa Idara ya Toba ya Kitume katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, Mapadre waungamishaji wanapaswa kukumbuka daima kwamba wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu na wala si watu mshahara! Ili kuweza kuadhimisha vyema Sakramenti ya huruma ya Mungu kuna haja ya kuwa na maandalizi mazito na majiundo makini katika: Taalimungu, Sheria za Kanisa na Shughuli za kichungaji, ili kuwawezesha kutekeleza dhamana hii nyeti katika maisha na utume wa Kanisa. Ili waamini wanaokimbilia katika Mahakama ya huruma ya Mungu, waweze kuonja ukuu wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili waweze kuendelea kumtumainia Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani!

Baba Mtakatifu Francisko mwaka 2017 aliitaka Idara ya Toba ya Kitume, kuangalia uwezekano wa kutoa mafunzo yatakayowasaidia Mapadre waungamishaji kutoa huduma kwa waamini wenye matatizo ya kiroho na yale yanayofanana sana na kupagawa na pepo wa wachafu, ili waamini kama hao wanapokwenda kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, waweze kupata huduma makini zaidi, baada ya kupima hali ya mwamini, ili aweze kupelekwa kwa wahusika zaidi. Mapadre wanapokuwa kwenye Kiti cha maungamo wawe: wapole, wanyenyekevu, wasikivu na watu wa sala. Mapadre waboreshe zaidi maisha yao kwa tafakari ya kina pamoja na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, wakitambua kwamba, wao ni watu wa kwanza wanaotakiwa kukimbilia huruma ya Mungu, ili kuweza kuiadhimisha vyema katika maisha na utume wao! Mapadre wawe ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili waamini waweze kuona ufunuo wa Uso wa Mungu katika huduma yao.

Huruma na upendo wa Mungu ni kati ya tema zinazofumbatwa katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye hapo tarehe 19 Machi 2018 anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 5 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa la Kristo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Maskini, Amani na Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni utashi wa Mwenyezi Mungu kwamba, watu wote waokolewe, ndiyo maana Baba Mtakatifu amekuwa akihimiza huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha na matumaini mapya kama ilivyotokea kwa Baba mwenye huruma, kumwonjesha Mpotevu huruma na upendo usiokuwa na mipaka! Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yameacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa watu wengi duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.