2018-03-01 11:43:00

Rais Joseph Kabila kukutana na vigogo wa UN na Umoja wa Afrika


Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Watu wa Congo ameridhia wito uliotolewa kwake na Bwana Antonio Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Bwana Moussa Faki, Kamishina wa Umoja wa Afrika wa kutembelea nchini DRC kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu nchini humo, unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Desemba 2018. Viongozi hawa wa kimataifa wataweza kukutana na Rais Kabila katika tarehe watakayopanga wao wenyewe.

Tangu mwaka 2017 viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wamekuwa wakitembelea nchini DRC ili kuitaka Serikali iliyoko madarakani kuhakikisha kwamba, inafanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika hapo tarehe 23 Desemba 2018, tarehe Ambato bado iko mashakani kwani hadi sasa Rais Kabila bado hajairidhia. Umoja wa wapinzani nchini DRC wamemtaka Kabila kutekeleza makubaliano ya amani yaliyofikiwa tarehe 30 Desemba 2016 kwamba, hatawania tena awamu nyingine ya uongozi kama Rais wa DRC. Kutokana na shinikizo la wananchi la kutaka Rais Kabila kuachia ngazi, hali ya kisiasa nchini DRC inaendelea kuwa tete sana! Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna idadi kubwa ya wananchi wasiokuwa na makazi ya kudumu kutokana na kuhofia usalama wa maisha na mali zao! Watoto wanaishi katika mazingira hatarishi kwa kukosa huduma msingi za elimu, afya na chakula bora!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.