2018-03-01 08:44:00

Mkutano mkuu wa uinjilishaji ulimwenguni kufanyika Arusha, Tanzania


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Uinjilishaji Ulimwenguni, utakaofanyika Jijini Arusha, Tanzania, kuanzia tarehe 8-13 Machi 2018; kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika Roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”. Huu ni mkutano utakaoyashirikisha kwa namna ya pekee kabisa Makanisa Barani Afrika, kama wenyeji wa mkutano huu wa kimataifa, unaofanyika wakati huu ambako kuna changamoto kubwa ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Makanisa Barani Afrika yatakuwa na fursa ya kutafakari kwa kina na mapana kuhusu utume na mchango wa Makanisa katika ulimwengu wa utandawazi.

Mababa wa Kanisa wataangalia kwa namna ya pekee: hali halisi ya Makanisa Barani Afrika; changamoto za kiekumene; athari za umaskini kwa familia ya Mungu Barani Afrika; haki jamii katika ujumla wake; utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wanaounda sehemu kubwa ya nguvu kazi Barani Afrika! Vita, kinzani na mipasuko ya kidini, kisiasa na kijamii mambo yanayokwamisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Afrika. Tema nyingine muhimu sana zitakazovaliwa njuga na viongozi wa Makanisa Barani Afrika ni athari za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linakiri kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko kubwa la idadi ya Makanisa ya Kikristo Barani Afrika! Haya ni mafanikio makubwa, lakini yanapaswa kuimarishwa kwa kujikita katika ushuhuda wenye mvuto unaosimikwa katika uekumene wa huduma, maisha ya sala, ushuhuda hata ule wa uekumene wa damu! Jambo la kusikitisha na kuona pia kwamba, Makanisa haya bado yanaendelea kukinzana, kiasi hata cha kupoteza utambulisho wake. Kumbe, Mababa wa Kanisa watakuwa na kazi ya ziada ya kuweza kubainisha utambulisho na utume wa Makanisa Barani Afrika kama sehemu ya mchango wake katika ulimwengu wa utandawazi. Mchango wa wanawake na vijana ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya Makanisa Barani Afrika.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, linawataka wajumbe wa Makanisa Barani Afrika kuhakikisha kwamba, Makanisa yanafumbata kwa namna ya pekee kabisa “Utume wa Kinabii unaokazia umoja wa Kanisa; haki, amani, utu na heshima ya binadamu”. Katika kipindi cha takribani miaka 50 ya Majadiliano ya kiekumene, Makanisa mbali mbali tayari yamejijengea uwezo wa kitaalimungu pamoja na nyenzo za kuganga na kutibu kashfa ya utengano kati ya Makanisa, ili kujenga umoja, mshikamano na upendo, chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu.

Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza kabisa, Mkutano wa Makanisa Ulimwenguni kwa Bara la Afrika, ulifanyika mjini Accra, Ghana kunako mwaka 1958. Mkutano huu, unafanyika tena Barani Afrika mwaka 2018 na Jiji la Arusha lenye vivutio vingi vya kitalii, limechaguliwa kuwa ni Mwenyeji wa mkutano huu, utakaofanyika kuanzia tarehe8 -13 Machi 2018; kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika Roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”. Mkutano mkuu wa mwisho, uliadhimishwa huko Athen, nchini Ugiriki, kunako mwaka 2005. Wajumbe 700 kutoka Makanisa mbali mbali duniani, watakausanyika Jijini Arusha ili kujifunza mbinu mkakati wa Makanisa Barani Afrika katika mchakato wa uinjilishaji na umissionari wa Makanisa, kama sehemu ya hija ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kuendeleza hija ya haki na amani iliyozinduliwa kunako mwaka 2013 kama sehemu ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia!

Watanzania wanaoheshimika kutokana na ukarimu na upendo kwa jirani zao, wanasubiri kuwakaribisha Mababa wa Kanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia nchini Tanzania, chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli, “Jembe la nguvu” katika kuwatetea wanyonge sanjari na ulinzi wa rasilimali za nchi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.