2018-03-01 10:23:00

Caritas Internationalis: DRC. Hali ni tete sana!


Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis linasema, baada ya familia ya Mungu kushiriki kikamilifu katika siku ya kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani, iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 23 Februari 2018 sasa kuna haja ya kupiga hatua kubwa zaidi, ili kuhakikisha kwamba, sala hii inamwilishwa katika matendo ya huruma! Vita, ghasia na mipasuko ya kijamii nchini DRC, inaendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia; maelfu ya watu kulazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao.

Matokeo yake: watoto wanakosa huduma msingi za elimu na afya, kiasi kwamba, wako hatarini kuambukizwa na magonjwa ya mlipuko na kwamba, wengi wao wanaishi katika mazingira hatarishi sana! Taarifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2018, kuna zaidi ya watoto milioni 2.2 ambao wanateseka sana kutokana na utapiamlo wa kutisha. Zaidi ya watu milioni 13.1 wanahitaji msaada wa dharura. Taarifa zinazonesha kwamba, kuna zaidi ya raia milioni 4 ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao. DRC ni nchi inayoongoza Barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na makazi maalum.

Askofu mkuu Marcel Utembi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC anasema, madhara ya vita na mipasuko ya kijamii nchini DRC yanaleta pia kero kwa nchi jirani ambazo zinapaswa, kimaadili kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka DRC. Ndiyo maana, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka Serikali iliyoko madarakani kuhakikisha kwamba, inadumisha utawala wa sheria na demokrasia ya kweli ili kulinda, kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake.

Kumekuwepo na mauaji ya makundi ya watu huko Ituri, Fizi na Bunia hali ambayo imesababisha hofu na mashaka makubwa miongoni mwa raia, kiasi cha kuyakimbia makazi yao ili kutafuta hifadhi. Taarifa ya Caritas nchini DRC inabainisha kwamba, makazi ya watu, nyumba na shule zimetiwa moto. Hospitali kwa sasa hazina tena dawa. Caritas Internationalis linasema, kwa sasa kuna maelfu ya wakimbizi na wahamiaji wanaohitaji msaada wa dharura, kwani wengi wao wanaendelea kuvuka mipaka ya DRC na kuingia: Tanzania na Burundi. Idadi ya vifo vya watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano inaendelea kuongezeka kila kukicha.

Eneo la Kasai lililokuwa na amani na utulivu mkubwa, lakini, tangu mwaka 2016  hadi mwaka 2017 limekuwa ni eneo la vita na kwamba, watu wengi wamepoteza maisha. Takwimu zinaonesha kuwa, watu zaidi ya milioni 1.5 wamekimbilia msituni na wanaishi katika mazingira magumu sana! Bado wanaogopa kurejea kwenye makazi yao. Caritas Internationalis inawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuisaidia DRC kwa hali na mali, ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia, wengi wao wakiwa ni watoto, wanawake na wazee. 

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka familia ya Mungu nchini DRC kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa njia ya amani. Wananchi watambue kwamba, mustakabali wa nchi yao; ulinzi na usalama viko mikononi mwao wenyewe. Maaskofu wanasikitika kusema, DRC inaendelea kuwa ni uwanja wa vita, ghasia na mipasuko ya kijamii, hali ambayo inahitaji toba, wongofu wa ndani; haki, amani na upatanisho wa kitaifa ili kuweza kuanza tena upya, kwa kujikita katika haki msingi za binadamu na utawala wa sheria na demokrasia ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.