2018-03-01 08:17:00

Baraza la Makardinali Washauri lamaliza kikao chake cha XXIII


Katiba ya Kitaalimungu ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Rasilimali watu, mchakato wa kubana matumizi Vatican pamoja na ulinzi wa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ni kati ya mada kuu zilizochambuliwa na Kikao cha XXIII cha Baraza la Makardinari Washauri lililoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 26 – 28 Februari 2018. Hayo yamebainishwa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican, Jumatano tarehe 28 Februari 2018.

Wajumbe wote wa Baraza la Makardinali Washauri wamehudhuria mkutano huu tangu mwanzo, isipokuwa Kardinali George Pell na Kardinali Laurent Pasinya Monswengwo aliyewasili kwa kuchelewa kidogo baada ya ndege aliyokuwa anatarajia kusafiria kufuta safari zake kutokana na hali mbaya ya hewa. Makardinali washauri wamejadili kwa kina na mapana: Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu; Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki pamoja na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Wamekazia kwa namna ya pekee, utekelezaji wa sera na mikakati iliyokwisha kupangwa kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, dhana ambayo inamgusa hata Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kuweza kutekeleza dhamana yake kwa uaminifu kadiri ya maagizo ya Kristo Yesu pamoja na kusoma alama za nyakati ili kukoleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Wongofu wa kichungaji ni muhimu, ili kuzaa matunda yaliyokusudiwa na Mababa wa Kanisa katika urika wa Maaskofu. Hapa changamoto ni kuhakikisha kwamba, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanatekeleza dhamana na wajibu wake barabara badala ya kulimbikiza majukumu yote kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hali inayogumisha maisha ya Kanisa pamoja na utekelezaji wa ari na utume wa kimisionari! Hii ni tafakari ya kina kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” namba 32.  Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yanapaswa kupewa uwezo na mamlaka kamili ya kufundisha. Lengo ni kugawanya madaraka.

Makardinali wameshauri kwamba, Waraka wa kitume uliochapishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1998 “Apostolos suos”, yaani “Asili ya Kitaalimungu na Kisheria ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki” uchambuliwe tena upya pamoja na kuhakikisha kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anaendelea kutekeleza dhamana ya kulinda na kudumisha umoja wa Kanisa. Makardinali pia wamemsikiliza kwa makini Askofu mkuu Jan Romeo Pawlowski, kuhusu maendeleo yaliyofikiwa kwenye kitengo cha tatu cha Sekretarieti kuu ya Vatican kuhusu uteuzi na majiundo kwa wanadiplomasia wa Vatican.

Kwa upande wake Kardinali Reinhard Marx amewasilisha mpango kazi na maendeleo yaliyofikiwa na Baraza la Uchumi la Vatican na kwa sasa linaendelea kufanya upembuzi yakinifu kuhusu rasilimali watu. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa kubana matumizi ya Vatican, ili kila senti inayotoka iweze kuchangia katika mchakato wa uinjilishaji mpya, daima kwa kuwa makini na gharama za uendeshaji wa shughuli na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Vatican imeendelea kuimarisha bajeti yake kwa kuwa na uwiano sawa wa mapato na matumizi. Taasisi mbali mbali za Vatican zinaendelea kuhimizwa kubana matumizi.

Baraza la Makardinali Washauri, limejadili pia kuhusu dhamana na utume wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa; umuhimu wa kushughulikia kesi za nyanyaso za kijinsia kwa haraka zaidi. Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, amewaelezea Makardinali kuhusu: mafanikio, changamoto na matarajio ya Baraza kwa siku za usoni. Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki pamoja na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu yamejadiliwa pia. Baraza la Makardinali litakuwa tena na kikao chake cha 24 kuanzia tarehe 23- 25 Aprili 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.