2018-02-28 14:27:00

Hekalu ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake!


Kabla ya kuendelea mbele, tujikumbushe tafakari katika jumapili zilizotangulia. Katika jumapili ya kwanza tulitafakari na kuongozana na Yesu akiwa jangwani. Jumapili ya pili, tukatafari na Yesu akiwa mlimani. Yesu anabadilika sura.   Katika jumapili hii ya leo, tunamkuta Yesu hekaluni. Ila hapa uso haung’ai bali yuko katika majonzi. Yesu anachukizwa na tabia ya ubinafsi iliyojengeka miongoni mwa viongozi wa dini. Hekalu liligawanyika sehemu tano (5):

  1. Sehemu takatifu – holy of holies
  2. Chemba ya makuhani – court of priests
  3. Chemba ya Israeli – court of Israelites
  4. Chemba ya wanawake – court of women
  5. Chemba ya wapagani – court of gentiles

Ni hii chemba ya wapagani waliyokuwa wakiitumia kama soko. Miili yetu imegawanyika katika viungo mbalimbali. Inawezekana pia badala ya kutumika kama hekalu la Roho Mtakatifu, ikatumika kama soko. Hatuna budi kutafakari vizuri. Hapa tunaona wazi kuwa matumizi sahihi ya hekalu yameharibiwa. Viongozi wa dini wameweka mbele ibada ya dini zaidi ya maadili na ubinafsi ukazidi. Viongozi wa hekalu walitilia mkazo kuona kuwa waliokuja hekaluni walipata wanyama wanono kwa ajili ya kutolea sadaka. Walihakikisha kuwa hata hiyo hela chafu iliyoletwa na waamini ilibadilishwa na ile hela ya hekalu. Kwa ajili hiyo wanapanga hata kumuua Yesu. Mahangaiko yao ni kumfurahisha Mungu lakini hawamjali Mwanae. Kwao kumfurahisha Mungu ni kitu cha kufanyia hekaluni, lakini hawakujali mahusiano yao na jirani. Hili ndilo linalomwudhi Yesu.

Ujumbe wa Kristo Yesu siku hii ya leo ni juu au habari ya uwepo wa ufalme wa Mungu. Wito ni kuwa na namna mpya ya matumizi ya iliyoitwa hekalu. Angalia Mk. 1:15 – wakati umefika, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini injili - na huu ndio ulikuwa utume wake Kristo – kuutangaza ufalme wa Mungu. Ufalme wa Mungu maana yake ni kuutakatifuza ulimwengu – kupatanisha yote katika Mwanae, kujenga mahusiano mapya, lakini tukikumbuka hali ya dhambi, yahitaji mapambano makali kabisa. Angalia katika Injili, Yesu aligeuza meza zao. Kwa hiyo yahitajika mapinduzi ya hali ya juu. Ila kila mapinduzi ya kweli, yanahitaji pia uwepo wa neema ya Mungu kama ilivyo katika somo la kwanza. Katika somo hili na ujumbe uliopo, twaona kwamba, Mungu anachukua jukumu. Mungu anafanya agano na watu wake. Anawapa amri zake ili waishi vizuri na kuupata uzima wa kweli. Kinyume na wito huu wa Mungu – itakuwa kilio kwao na kwa taifa zima  la Israeli.

Bahati mbaya na sababu ya hali zetu za kibinadamu, huu ufalme haueleweki kwa urahisi. Angalia somo la pili la leo. Hekima yake ni kuu kuliko yetu, udhaifu wake una nguvu kuliko udhaifu wetu. Leo twaalikwa kuikimbikia hiyo hekima ya Mungu ili tuweze kuyajua mapenzi yake. Walioishi kadiri ya hekima ya Mungu, waliokoka. Wanaobaki katika hekima zao wamepata maangamizi. Amani ni hali ya moyo na akili kabla ya kuwekwa katika mpangilio wa matendo, ndivyo hivyo ukristo wetu unavyotakiwa kuanza na mapinduzi ya mioyo yetu na maisha yetu. Ndicho kinachotakiwa katika kipindi hiki cha kwaresima. Kwa njia hii tunatambua ufalme wa Mungu na kufahamu tufanye nini katika kuujenga. Tutakuwa tayari kupindua maisha yetu juu chini ili kuanza upya. Ndiyo metanoia ya kweli, yaani: toba na wongofu wa ndani.

Hebu mfano huu utupatie changamoto kidogo – padre anavamiwa njiani na jambazi. Huku jambazi akishika kisu tayari kuua anadai fedha. Alipoendelea kumkaba koo mara alama ya vazi lake la kipadre ikaonekana kwani alikuwa amevaa koti zito sababu ya baridi kali. Mara jambazi akamwuliza – wewe ni padre? Naye akajibu ndiyo na kuwa alikuwa ametoka kumtembelea mgonjwa. Basi nenda. Akasema yule  jambazi. Hata hivyo padre akashangazwa kidogo na hali ya baridi iliyokuwa imembana yule jambazi. Kama namna ya kumsaidia, yule padre akataka kumpatia sigara avute, apate kujipasha joto kidogo. Yule jambazi akajibu haraka haraka, padre hapana. Nimefunga sigara, hii ni Kwaresima. Ona jinsi jambazi anavyoshika jambo moja tu la uchaji lakini anasahau amri kuu na ya msingi – usiue. Yawezekana pia sisi tukaishika Kwaresima kwa mtindo kama wa huyu jambazi. Yahitajika kufayanya mapinduzi ya kweli, yaani toka ndani kabisa ya mioyo na maisha yetu.

Tumsifu Yesu Kristo.                           

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.