2018-02-28 13:55:00

Askofu Amon Kinyunyu: Changamoto ni muhimu ili kuleta maendeleo


Askofu Amon Kinyunyu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri  Tanzania (KKKT)   Dayosisi ya Dodoma  amesema kuwa mauaji na uvunjifu wa haki msingi za binadamu unaoendelea kutokea nchini Tanzania ni matokeo ya  wivu, uchu wa mali na  madaraka pamoja na tabia ya watu kutokupenda mabadiliko. Kauli hiyo ameisema hivi karibuni wakati akihubiri kwenye Ibada ya uwekaji wa jiwe la msingi  la Kanisa la  Kiinjili Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Dodoma. Gharama za ujenzi hadi kumalizika kwake, inakadiriwa kufikia zaidi ya milioni 826. Ibada hii  ilifanyika katika Usharika wa Nkuhungu, Dayosisi ya Dodoma. Askofu Kinyunyu alisema  kuwa mauji hayo yanayotokea  katika  jamii, yanachangiwa na wivu wa kutopenda maendeleo na  hii inasababishwa na watu kujisahau katika kumtumainia na kumtumikia Mwenyezi Mungu.

Akihubiri katika ibada hiyo alisema kama jamii itaendelea kuwa na uchu wa mali na madaraka hakuwezi kuwepo maendeleo yoyote kwani watu watakuwa wanafanya vitu kwa kunung’unika na kudai kuwa  hakuna mabadiliko yasiyokuwa na makwazo. “Lazima kwenye mabadiliko kuna watu watachukia, watakwazika  mabadiliko hatujaanza sisi mabadiliko yalianza kwa Wayahudi lolote linalofanywa katika ulimwengu huu lazima tukumbuke neema ya Mungu, Mabadiliko yanapotokea  hii inatupelekea kuona ni namna gani tuanamwabudu Mungu wetu,’’alisema Kinyunyu.

Akizungumzia kwa upande wa serikali alisema, kwa kuwa Dodoma sasa ni makao makuu  ni jukumu la waumini wote na jamii kiujumla kubadilika ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano  na kuleta Mabadiliko katika Mkoa wetu. “Tusipojiweka sawa kama kanisa  Serikali itatupita na kama ikitupita basi tutakuwa kama kipofu aliyekosa mtu wa kumwongoza,’’ aliongeza Askofu. Hata hivyo, aliwataka waamini kuvaa mavazi ya heshima wakati wa ibada ili kuendelea kumheshimu, kumtukuza, kumwomba na kumsifu Mwenyezi Mungu, Baba yetu aliye mbinguni kwani Mwenyezi Mungu ni Baba wa heshima. ‘’Mungu wetu ni Mungu wa heshima tuvae mavazi ya heshima ili tuonyeshe mwonekano mzuri kwa Mungu wetu,’’aliendelea kuongeza Askofu Kinyunyu.

Naye Katibu wa Ujenzi wa kanisa hilo Emmanueli Ngilangwa akitoa taarifa fupi kwa waamini alisema kuwa Kanisa hilo lilianza kujengwa  mwezi Machi 2016 huku akisema kuwa  zaidi ya shilingi milioni 826 zitatumika katika  kukamilisha jengo hilo. Mbali na hayo alisema, miongoni mwa changamoto wanazipata katika ujenzi wa kanisa hilo ni pamoja na  gharama ya vifaa kupanda kila siku ikiwemo na usimaminzi wake. "Hata hivyo sisi kama watu wake Mwenyezi Mungu, naamini na matumaini yetu ni muhimu tukamwamini kuwa ujenzi huo utakamilika kwa kuwa Mungu wetu atafanya matendo makuu" Alisema Ngilangwa. Katika ibada hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi la Kanisa hilo uliambatana na harambe iliyofanywa kwa lengo la kupata milioni 18 ambazo zitakazowezesha kufunga  leta. Kanisa hilo  linalojengwa litakuwa linachunguwa zaidi ya waumini elfu 2000 watakao kuwa wanatumika kuabudia ikiwemo na huduma mbalimbali za kirohona kijamii.

Na Rodrick Minja, Dodoma.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.