2018-02-27 14:33:00

Watoto zaidi ya 90, 000 wamelazimika kuzikimbia familia zao, DRC


Msikilizaji, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF, limeingiwa na wasiwasi mkubwa na limetoa taarifa rasmi kuhusu kulazimika kukimbia kwa watoto wanao karibia 90,000 elfu kutoka jimbo la ITURI, kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Watoto hawa ni wale wanaokimbia ghasia, vita, kinzani na umaskini. Eneo la DJUGU, huko Kaskazini Mashariki mwa DRC, limekuwa ni sehemu ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na wengi wao wamejikuta hawana tena makazi kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao. UNICEF imetangaza kwamba hivi karibuni ghasia za kikabila katika jimbo hilo zimewakosesha makazi  watoto 66,000 ndani ya eneo hilo na kusababisha watoto wengine 25,000 elfu kutafuta hifadhi katika nchi jirani ya Uganda.

Ghasia hizi zilipamba moto kuanzia mwezi wa Februari mwaka huu,  na inasemekana kuwa karibu vijiji 70 vilichomwa moto, na zaidi ya watu 76 walipigwa risasi na kufa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.  Kuna ukosefu mkubwa wa huduma za Afya na elimu. Baadhi ya vituo vya afya na shule zimechomwa moto na hivyo kuwanyima watoto hao fursa ya kupata elimu.  Watoto wengi waliokimbia kutoka DRC wamepewa hifadhi ya muda kwenye shule, makanisa na ndani ya hospitali zilizoko karibu na jiji la BUNIA ambao ni mji mkuu wa ITURI.

UNICEF inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwalinda watoto hawa, kuwapatia elimu, huduma za afya pamoja na kuzitaka serikali kushughulikia chimbuko linalo chochea watu kuzihama nchi zao.  Pia Viongozi wa Kimataifa wametakiwa kuongeza juhudi za kuhakikisha familia zinaishi pamoja na kujizuia kuwashikilia watu vizuizini ili kupunguza idadi ya watoto wanaojikuta peke yao katika mazingira hatarishi wanapo kimbia vita, na kuchukua hatua za haraka kutafuta ufumbuzi ili kutatua tatizo hili. UNICEF inaripoti kuwa takriban watoto 90,000 wamelazimishwa kukimbia makazi yao kutokana na vita pamoja na ghasia . UNICEF imeonya kwamba maelfu ya watoto wako hatarini  kukumbwa na ugonjwa wa Kipindupindu na maradhi mengine ya kuambukiza kwa sababu ya hali mbaya ya hewa, ukosefu wa chakula na maji safi. UNICEF inatoa wito wa kupatikana kwa suluhisho la amani kwa mzozo, na kuelezea kuwa kumalizika kwa ghasia ndiyo njia pekee ya kuwalinda watoto kutokana na hatari nyingi wanazo kabiliana nazo. 

Na Pauline Mkondya,

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.