Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Elimu

Msipotubu, kuongoka na kubadilika, mtaendelea kuwa "makinikia"!

Mafumbo ya Kanisa mnayoadhimisha na kushiriki yawaletee waamini utakatifu wa maisha!

26/02/2018 13:43

Padre Alcuin Nyirenda, OSB, amewataka waamini kutumia vyema kipindi hiki cha Kwaresima kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuambata utakatifu wa maisha. Kiwe ni kipindi cha kupanda kwenda Mlimani kukutana na hatimaye, kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka inayong’ara kwa harufu ya utakatifu wa maisha, kama ilivyokuwa kwa Mzee Abrahamu, Musa, Wayahudi na Yesu katika Agano Jipya, kama anavyosimuliwa kwenye Injili ya Marko, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima. Haya yanapaswa kuwa ni matunda ya juhudi binafsi katika kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha, kwa kuwa na uthabiti wa moyo, tayari kukabiliana na changamoto za maisha!

Padre Nyirenda ameyasema hayo, Jumapili tarehe 25 Februari 2018, wakati wa mahubiri yake Ibada ya Misa Takatifu  kwa ajili ya Jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki Watanzania Wanaosoma na kuishi Roma, iliyoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Makao Makuu ya Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia.  Imekuwa ni fursa kwa ajili ya kuombea viongozi wa Tanzania na raia wake wote: umoja, haki, amani, upendo, mshikamano wa kitaifa na uzalendo wa kweli, msamaha pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wapya wa Jumuiya hii.

Yesu baada ya kuwapatia Mitume wake ”Sala kuu ya Baba Yetu” kama mwongozo wa maisha na ”Heri za Mlimani” kama ”Katiba” aliwaona wakianza kugombania madaraka kati yao, ndiyo maana akawachukua baadhi yao faragha na kuanza kugeuka sura mbele kama kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii, tendo ambalo lilishuhudiwa na Mtakatifu Petro, Yohane na Yakobo. Yesu alipenda kuwaambia mapema wafuasi wake kwamba atauwawa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu! Yesu alipokuwa pale farghani aliwaonesha utukufu wake na kama ilivyoaguliwa katika Torati na Manabii atapata utukufu wa ufufuko kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake.

Kipindi cha Kwaresima kiwasaidie waamini kupata mang’amuzi ya mambo msingi katika maisha yao ya imani, ili waweze kugeuka na kubadilika. Maadhimimisho ya Mafumbo ya Kanisa iwe ni chachu ya kukoleza mabadiliko haya ya maisha yanayojikita katika utakatifu wa maisha. Kwa wanafunzi, mang’amuzi haya mapya yajikite katika kile wanachojifunza ili kiwaletee mabadiliko ya kweli katika maisha. Kama wanasomea sayansi ya Maandiko Matakatifu, wasaidia kumng’arisha Kristo Yesu kwa watu wake! Kama ni wanataalimungu, yaani waalimu wa Kanisa, watambulikane kwa kile wanachofundisha na kuadhimisha, ili hatimaye, wawe ni dhahabu na almasi inayong’aa katika huduma! Haya ni mapambano ya kweli yanayopaswa kuvaliwa njuga na waamini wote.

Wakati huo huo, habari kutoka Jimbo Katoliki la Geita zinasema kwamba, Rais John Pombe Magufuli, Jumapili tarehe 25 Februari 2018 amehudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia teule ya Mlimani iliyokuwa inaongozwa na Padre Alex Bulandi. Baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Rais Magufuli amechangia kiasi cha shilingi milioni mbili ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Parokia hiyo teule. Amewataka watanzania kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Pili watanzania wapendane na kuheshimiana. Amekiri kwamba, kazi yake kama Rais si lelemama inahitaji kusindikizwa kwa sala na sadaka ili kweli aweze kutekeleza wajibu wake kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

26/02/2018 13:43