Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Maaskofu: Nigeria inapekenyuliwa sana na utamaduni wa kifo!

Utamaduni wa kifo unapekenyua maisha ya watu wengi nchini Nigeria. - REUTERS

26/02/2018 13:27

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, (CBCN) katika kikao chake cha mwaka kilichofanyika huko Abuja, kuanzia tarehe 17 - 23 Februari 2018; pamoja na mambo mengine, kimekazia umuhimu wa kusimama kidete katika kudumisha uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; Kanisa na Ujasiria mali; vijana na uzalishaji; dhamana na wajibu wa Serikali; uandikishwaji wa kura; matukio mbali mbali ya Kikanisa ndani na nje ya Nigeria; mambo yote haya yanahitaji kusimikwa katika moyo wa upatanisho na amani! Askofu Mkuu Augustine Obiora Akubeze wa Jimbo kuu la Benin City, amechaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria na hivyo kuchukua nafasi ya Askofu Mkuu Ignatius Ayau Kaigama aliyemaliza muda wake. Wakati huo huo, Askofu Camillus Raymond Umoh wa Jimbo Katoliki la Ikot-Ekpene amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini humo kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kutambua kwamba, maisha ni matakatifu, zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, fumbo kubwa na changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga. Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na matukio ya mauaji ya wanasiasa na watu wasiokuwa na hatia na hasa zaidi vijana. Maaskofu wanakaza kusema, hakuna taasisi au mtu mwenye dhamana ya kuondosha uhai wa mwingine. Kumbe, kuna haja kwa wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama kushikamana zaidi ili kuokoa maisha ya watu na kwamba, imeandikwa “Usiue”!

Maaskofu wanaonesha wasi wasi wao kuhusu Muswada wa sheria ya usawa wa kijinsia na haki sawa, unaoweza kutumiwa kama kificho cha utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera na utoaji mimba na mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Inasikitisha kuona kwamba, Serikali inataka kuhalalisha ngono shuleni, kwenye taasisi za elimu na vituo vya afya kwa kuwagawia wanafunzi kondom na vizuia mimba, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuwa makini na kamwe wasitumiwe kuwa vichokoo vya anasa za dunia hii. Wazazi wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao wa malezi na majiundo makini kwa watoto wao. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kujikita zaidi na zaidi katika imani na mshikamano wa udugu na upendo. Maaskofu wa Nigeria wanasikitika kusema kwamba, ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na wafanyakazi waliostaafu kazi kujikuta wametelekezwa kama gari bovu ni mambo yanayotia shaka na wasi wasi kwa ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Nigeria. Makundi haya ni sawa na bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa jamii. Wafanyakazi waliostaafu, wajishughulishe kutafuta fursa nyingine zitakazowawezesha kuendelea kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa kujihusisha na kazi halali, ili kweli haki, amani na maendeleo yaweze kutawala. Kilimo kiboreshwe zaidi ili kutoa ajira kwa watu wengi zaidi.

Vijana wanaunda sehemu kubwa ya wananchi wa Nigeria na kwamba, Kanisa na jamii inawatarajia vijana kuchangia zaidi katika shughuli za uzalishaji kwa kuhakikisha kwamba, wanajipatia kipato chao kwa shughuli halali pamoja na kutumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi wa wengi. Vijana watambue kwamba, kazi ni kipimo cha utu na heshima ya binadamu, changamoto na mwaliko kwa vijana kuondokana na tabia ya uzembe na badala yake, watumie nguvu zao katika huduma na uzalishaji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linamshukuru na kumpongeza Rais Muhammady Buhari kwa kuwapokea na kusikiliza maoni yao. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, maoni yao yatasikilizwa na kufanyiwa kazi kwa ajili ya mustakabali wa familia ya Mungu nchini Nigeria. Lengo ni kuboresha hali ya maisha ya wananchi wengi; kuunda mazingira ya uzalishaji wa ajira, kuboresha miundo mbinu na huduma mbali mbali za kijamii na kiuchumi; lakini zaidi kwa kuzingatia utawala bora unaosimikwa katika: Katiba, sheria na kanuni. Wanawahimiza wananchi wa Nigeria kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria litakuwa na Hija ya Kitume “Ad Limina Visit” inayofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hija hii itaanza hapo tarehe 15 Aprili hadi tarehe 5 Mei 2018. Itakuwa ni nafasi ya kukaa na kujadiliana na Khalifa wa Mtakatifu Petro kuhusu maisha na utume wa Kanisa nchini Nigeria pamoja na changamoto zake. Maaskofu watapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Vatican. Kanisa nchini Nigeria linajiandaa pia kushiriki kaikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakaofanyika kuanzia tarehe 3 - 28 Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani, Mang’amuzi ya Miito”. Maaskofu wanasikitishwa sana na kitendo cha baadhi ya wakleri na waamini kushindwa kumpokea Askofu mstaafu Peter Okpaleke kama mchungaji mkuu wa Jimbo Katoliki la Ahiara, jambo linalowataka kutubu, kuongoka na kujipatanisha na Mungu pamoja na Kanisa ili amani iweze tena kurejea Jimboni humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

26/02/2018 13:27