Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Dini zisaidie mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu!

Dini mbali mbali hazina budi kuchangia katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa kuzingatia kanuni maadili, utu, heshima na haki msingi za binadamu! - REUTERS

26/02/2018 14:08

Dini mbali mbali na kwa namna ya pekee dini ya kikristo yenye mizizi yake kutoka dini ya kiyahudi, zina kusanyiko wa kanuni za kimaadili, lakini pia zinatoa fursa kwa binadamu kuwa na mahusiano binafsi na Mweza wa Yote. Mwenyezi Mungu ambaye Neno na Hekima yake vinaikumbutaia na kuipenya dunia, ndiye Yeye anayeifahamu vema na kuuongoza ulimwengu katika wema. Hivyo kila tafiti, elimu, ufahamu, na sayansi havipaswi kuwa vinafanyika hewani hewani, bali vinapaswa kufanyika katika muktadha wa hekima na upendo wa kimungu. Kwa namna hii, mnamo tarehe 29 Januari 2018, ndivyo ilivyosikika sauti ya Kardinali Peter Erdö, Askofu mkuu wa Esztergom-Budapest, ikichana mawimbi katika ukumbi wa Chuo kikuu cha Colombia Jijini New York, alipokuwa akiongelea nafasi ya dini katika jamii ya kisekulari, yaani Jamii isiyomwamini Mungu.

Baadhi ya mawazo na mafundisho msingi ya dini na tamaduni za kikristo kama vile ulazima wa kuivumbua zaidi dunia isiyoonekana kwa macho na uelewa mpana wa dunia inayoonekana, ni kati ya dhana chanya zinazoonesha mahusiano mazuri kati ya dini, historia na sayansi. Sayansi leo hii inaendelea kujipambanua kwa ufahamu-bunifu unaendana na taratibu zilizopangwa vizuri zinazouendesha ulimwengu. Kardinali Peter Erdö anasema, kanuni maadili zinaweza kuwa nyingi na zinazotofautiana kiasi, lakini ni muhimu kutambua kwamba, kanuni hizi lazima ziende sambamba na uhalisia wa mambo, uchambuzi na upangaji wake katika kweli na sio kukurupuka tu kufuata hisia, maslahi au matamanio ya watu fulani fulani.

Kardinali Peter Erdö anasema, kunaweza kuwepo na nia ya kutafuta majibu ya changamoto za sasa kutokana na mafundisho ya halakhah, yaani mkusanyiko wa sheria za Torah ya kiyahudi iliyoandikwa, pamoja na Taalmud, tamaduni zilizorithishwa kwa mdomo na uchambuzi wa Marabi; au kunaweza kuwa na kudai ruhusa ya kuimba haggadah, yaani ibada na nyimbo za kiyahudi kusherehekea ukombozi wao kutoka utumwani kwa mkono wa nguvu wa Mungu. Haya yote ni sahihi kufanya, sababu hata Kristo alilazimika kutumia taratibu za kanuni maadili katika kufundisha, kiasi cha kuwarithisha wanafunzi wake ishara kubwa za wakati wa uhai wake kama vile karamu ya mwisho, fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi (Rej., Luka 22:19) .

Changamoto zinazoonekana leo ni uhalisia kwamba kila siku maendeleo ya sayansi na teknolojia na hata sayansi asili, yanaibua mambo mapya kila siku ambayo yanahitaji kutafutiwa majibu iwapo yanaendana kweli na kanuni maadili. Kardinali Peter Erdö anaalika dini zote kutokukata tamaa wala kuchoka kuhakikisha zinachambua kwa kina na kutoa misimamo ya kimaadili kwa kila hali au mfumo wa maisha unaoibuliwa kila mara, hata kama wapo watakaopinga, kugoma au kulaumu. Hili lifanyike kwa kuzingatia Nyanja zote, kiutu, kiuchumi, kisayansi, kisiasa, kijamii, na kimazingira Nyumba ya wote.

Kardinali Peter Erdö anasema, ni imani yake kubwa ya kwamba taalimungu za dini nyingi zina ufanano wa namna fulani, hasa kwenye kumtambua Mwenyezi Mugu Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana; Mungu ambaye anavitambua kuwa ni vema iwapo vinatunzwa na vinatumika kwa kufuata kanuni maadili (Rej., Mwanzo 1:31). Mungu huyu anatambulika kuwa ni mwema na mwenye huruma, anayejifunua kwa binadamu na kujenga uaminifu kwa mtu binafsi na kwa jumuiya katika ujumla wake. Kwa sababu hiyo, tafiti na uelewa wa binadamu usikate tamaa sababu ya udhaifu na mipaka ya binadamu, bali binadamu wote wajiaminishe katika hekima na upendo wa Mungu mwaminifu, na siku zote kuzingatia maagizo yake katika tunu msingi za maadili.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

26/02/2018 14:08