Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Wakristo fungeni na kusali katika roho na kweli!

Kwaresima iwe ni fursa ya kutafakari mateso, kifo na ufufuko ili kuonesha toba na wongofu wa ndani, tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: haki, amani na maridhiano kati ya watu. - AP

24/02/2018 09:25

Kanisa ni  Fumbo la Mwili wa Kristo. Kila mwamini ni kiungo cha mwili huu mmoja ambapo Kristo Yesu ndiye kichwa (Rej., Lumen gentium 7). Hivyo kila furaha ya mmoja ni furaha ya mwili mzima, na kila mateso na dhuluma kwa mmoja ni mateso na dhuluma kwa wote: “Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho” (IWakorintho 12:26). Ndio sababu, Sauli alipowatesa wakristo kabla ya wongofu wake, anapokutana na Kristo njiani kuelekea Damasko anamuuliza Kristo kuwa ni nani, Naye anamjibu: “Mimi ndimi Yesu unayemtesa” (Matendo 9:5). Jibu la kristo ni uthibitisho ya kuwa mateso ya waamini, yanamuumiza, sababu ni viungo vya mwili wake. Kanisa limeunganishwa katika umoja madhubuti wa Utatu Mtakatifu (Rej. Lumen gentium 4).

Wapo wakristo wengi wanaoteseka na kudhulumiwa sehemu mbali mbali duniani. Wapo wanaoteswa wazi wazi kwa sababu ya imani yao kwa Kristo. Mfano wakristo wa maeneo ya Mashariki ya kati, China, Nigeria na kadhalika. Wapo pia waamini wanaoteseka sio sababu ya imani yao moja kwa moja, bali wakiwa sehemu ya wanyonge wengi kwa sababu za kinzani za kisiasa, kiuchumi, na kijamii. Mfano wa mateso na dhuluma hizo ni pamoja na sehemu za Somalia ambapo wengi wanafariki kwa njaa; Sudani ya kusini kwa ghasia za ukabila; DRC kwa vurugu za uchu wa mali na madaraka.

Aidha kuna uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu leo hii, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo yanayopelekea mabinti wadogo na wanawake kwa ujumla kutumiwa kama vyombo vya kukidhi tamaa za ngono; vijana kuchukuliwa baadhi ya viungo vyao na vinafanyiwa biashara; kufanyishwa kazi kwa ujira mdogo na kadhalika. Haya yote ni mateso na dhuluma ambavyo vinaendelea kuutesa mwili wa Kristo.

Kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha kuadhimisha fumbo la wokovu wa mwanadamu kwa njia ya mateso,  kifo na ufufuko wa Kristo. Fumbo la Pasaka, ni fumbo linalomkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa shetani, utumwa wa dhambi na mauti. Kabla ya wokovu huu, mwanadamu alikuwa anaburuzwa na kugaragazwa vibaya na Ibilisi katika udanganyifu, na hivyo kujikuta akitenda dhambi nyingi kwa kuhadaika. Yeyote anayeendekeza dhambi, anabaki kuwa mtumwa wa shetani: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa uongo” (Yohane 8:44).

Yohane mbatizaji hali akimuandalia Bwana njia ahubiri akisema: “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvilegeza viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Mathayo 3:11). Kwa ubatizo wa Roho Mtakatifu, Kristo anamwongoza mwanadamu kuufahamu ukweli, ili asihadaike kwa kutenda yaliyo hila za shetani. Bwana asema: “Ninyi mkikaa katika Neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru” (Yohane 8:31-32). Ukweli huu ndio unaomweka mwanadamu huru, ukweli unaomwezesha mwanadamu kufanya maamuzi kwa kutambua uchaguzi anaoufanya. Kwa sababu hiyo, mwanadamu anapoichagua dhambi, anakuwa ameamua kuwa mtumwa wa shetani, kwa kuwa “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi” (Yohane 8: 34).

Fumbo hili la Pasaka limemfinyanga mwanadamu kuwa kiumbe kipya (Gaudium et spes 22); na kupitia Kanisa, Kristo anamshirikisha mwanadamu Neema na Kweli (Lumen gentium 8). Kipindi hichi cha mfungo na sala, ni mwaliko kwa waamini kujitathimini iwapo wameupokea wokovu huo ambao Mwenyezi Mungu aliupania kwa ajili ya binadamu. Baada ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, Mungu kautenga muda ili Habari Njema ya wokovu huu iwafikie wanadamu wote katika kweli. Muda huu ambao Mwenyezi Mungu kautenga kabla Kristo hajarudi kutoa hukumu ya mwisho, ni muda na nafasi kwa binadamu kufanya uchaguzi sahihi, uchaguzi wenye ufahamu; kwani Mungu mwokozi wetu “anapendelea zaidi watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli” (ITimotheo 2:4. Rejea pia Lumen gentium 16).

Dhamiri na uhuru ambao mwanadamu kapewa na Mwenyezi Mungu una thamani kubwa machono pa Mungu, naye humuheshimu mwanadamu katika uchaguzi wake huku akimwangazia na kumsubiri kwa hamu aifuate njia iliyo sahihi (Rej., Gaudium et spes 14). Lakini kila uchaguzi una matokeo yake, ambayo mwanadamu atapaswa kuwa tayari kukabiliana nayo, hapa duniani na katika hukumu ya mwisho (Rej., Gaudium et spes 4). Hivi ndivyo ilivyompendeza Mwenyezi Mungu katika hekima yake kuu, kuacha wema na uovu kuwapo kwa pamoja, ili mwanadamu afanye uchaguzi kwa uhuru: “Akasema, La! Msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue pamoja hadi wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, yakusanyeni kwanza magugu myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu” (Mathayo 13: 29-30).

Kila dhambi ina matokeo yake ambayo yanamwandama mwenye kuitenda tangu angali hapa duniani. Mtume Paulo anapofundisha “kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23), haishii kwenye kifo cha roho kutengana na mwili, bali ni fundisho kwamba dhambi inamtenga mwanadamu na Neema zitokazo kwa Mungu. Ndio sababu Mtume Paulo huyo huyo anasema “wote wametenda dhambi na kupungukiwa utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23). Mwanadamu anapoukosa utukufu na neema ya Mungu, anapungukiwa nguvu thabiti ya kiimani kukabiliana na changamoto, hivyo anakuwa hatarini zaidi kuyumbishwa na lolote. Uhakika na usalama wa maisha yetu umo ndani ya Mwenyezi Mungu “kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uzima wetu” (Matendo 17:28).

Mbali ya matokeo ya dhambi ya muda hapa duniani. Kuna matokeo yale ya milele, kwani “Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili kumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele” (IWathesalonike 4: 16-17). Mtume Paulo anawapa tumaini waamini juu ya ufufuo wa wafu, na jinsi tendo hilo litafanyika kwa namna iliyojaa utukufu na ukuu wa Mungu. Kristo mwenyewe alilihakikisha hilo juu ya hukumu wa mwisho: “Msistaajabu maneno hayo, kwa maana saa inakuja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake (mwana). Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu” (Yohane 5:28-29). Kumbe hapa ndipo itakuwapo hukumu ya mwisho ya hakimu mwenye haki, mbali ya matokeo ya kila dhambi tunazotenda wanadamu, iwapo hatutaongoka hukumu hiyo ya mwisho itatupeleka katika moto wa milele. Hapo sasa hakutakuwapo tena uovu, maumivu, njaa, wala chuki; bali tutaishi kwa furaha na Amani hata milele.

Leo hii Mwenyezi Mungu anapenda haki itendeke na mwanadamu aishi kwa Amani. Lakini anapenda mwanadamu mwenyewe ashiriki katika mpango huo wa Mungu, wa kuijenga Jumuiya ya wanadamu yenye upendo. Hawa washiriki wa kuijenga Jumuiya ya binadamu namna hiyo, ndio watakaopokea thawabu hiyo ya kuurithi Ufalme wa milele, ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na Amani (Rej., Utangulizi wa Sikukuu ya Kristo Mfalme). Ufalme huu umekwishakusimikwa ndani ya nyoyo za watu kwa walio tayari. Na ndio sababu vigezo vya kushiriki katika ukamilifu wake vinaendana na namna tulivyo tayari kuushiriki ufalme huo hata sasa: “Njooni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nilikuwa na kiu mkaninywesha; nilikuwa mgeni, mkanikaribisha; nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nilikuwa kifungoni, mkanijia” (Mathayo 25: 34 – 36). Kila tunapotenda jema au baya kwa mmoja wapo wa wanyonge, tunakuwa tumelitenda kwa Kristo mwenyewe, kwani wanyonge hao ni viungo vya mwili mmoja wa Kristo (Rej., Mathayo 25:40;45. IWakorintho 12:12-31).

Na Padre Celestine Nyanda.

Vatican News!

24/02/2018 09:25