2018-02-24 13:02:00

Huduma ya uzuri iwe ni chemchemi ya ushuhuda wa imani na mapendo


Huduma ya uzuri Kikanisa ilianzishwa kunako mwaka 2012 kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa daraja ya mahusiano kati ya wasanii na Mwenyezi Mungu, ili wasanii hawa waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uzuri na utakatifu wa Mungu katika maisha yao. Ushemasi wa uzuri unawaunganisha: wanamuziki, washairi, waimbaji, wachoraji, wasarifu wa majengo, waigizaji na wachezaji ambao wanajitahidi katika maisha yao kudumisha kifungo cha upendo wa Jumuiya ambao unawawezesha kutafuta na kuambata ukweli katika maisha.

Huduma ya uzuri inajengeka katika mambo makuu manne: Sala, Ushuhuda, Malezi, Mshikamano na Mapumziko ya pamoja. Wajumbe wa Ushemasi wa uzuri kuanzia tarehe 18 hadi 25 Februari 2018 wana adhimisha kongamano, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Mwenyeheri Angelico inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 18 Februari. Katika maisha yake alijulikana kama Guido Pietro na baadaye akafahamika zaidi kama Fra Angelico, Msanii kutoka Italia aliyetangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya sanaa ya uchoraji. Kongamano hili limefunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 24 Februari 2018 amekutana na kuzungumza na washiriki wa kongamano hili. Ametumia fursa hii kuwapongeza kwa jitihada zao zinazopania kung’arisha uzuri wa kazi ya uumbaji kwa njia ya karama na mapaji yao pamoja na ushuhuda wa upendo na mshikamano wanaouonesha kwa wanyonge na maskini ndani ya jamii. Amewakumbusha kwamba, uzuri ni wito unaobubujika kutoka kwa Muumba na kuwa hii ni karama inayopaswa kufanyiwa kazi ili kuzaa matunda zaidi kama alivyowahi kukumbusha Mtakatifu Yohane Paulo II.

Huduma ya uzuri anasema Baba Mtakatifu Francisko, ni huduma iliyoanzishwa kunako mwaka 2012 wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Uinjilishaji mpya; kumbe, kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa safari kubwa iliyokwisha kufikiwa tangu wakati huo pamoja na wingi wa karama ambazo Mwenyezi Mungu amewasaidia kukuza kwa ajili ya huduma makini kwa jirani na binadamu wote katika ujumla wao. Karama ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mmoja wao ni wajibu na utume unaopaswa kufanyiwa kazi katika hali ya unyenyekevu bila kutafuta umaarufu au faida binafsi katika ulimwengu ambamo utaalam unaonekana kuwa kama rasilimali inayotoa maana na tafsiri ya maisha ya mtu.

Wajumbe wa huduma ya uzuri wanaitwa kwa njia ya karama pamoja na kuchota utajiri wa tasaufi ya maisha ya Kikristo kuwa na mwelekeo chanya mintarafu ubora wa maisha unaohimiza mtindo wa maisha ambao ni wa kinabii na kitaamuli, ili kupata furaha ya kweli katika maisha bila kumezwa na malimwengu. Wawe ni vyombo vya huduma ya kazi ya uumbaji, wakijitahidi daima kulinda “chemchemi ya uzuri” katika miji ambayo imezingirwa na kuta bila ya kuwa na roho! Baba Mtakatifu anawataka wasanii hawa kukuza na kudumisha karama na vipaji vyao ili kusaidia mchakato wa “wongofu wa kiekolojia” unaotambua na kuthamini utu na heshima ya binadamu; kwa kukuza kipaji cha ubunifu, ili kulinda ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato wa kutafuta uzuri na ubora wa maisha kati ya watu, usaidie pia kuweka uwiano bora wa utunzaji bora wa mazingira, utamaduni wa watu kukutana pamoja na kusaidiana.

Huduma ya uzuri iwe ni fursa ya kukuza utamaduni wa watu kukutana kwa kujenga na kudumisha madaraja kati ya watu, ili kubomolea mbali kuta zinazowatenganisha watu kutokana na sababu mbali mbali. Michezo yao iwe ni ushuhuda unaofumbata imani kwa Kristo Yesu, tayari kumfuasa kama jambo la kweli, haki na zuri linaloweza kuzima kiu ya furaha ya undani wa maisha ya mwanadamu licha ya fadhaa na majaribu katika maisha. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, anapenda kukazia kwa kusema kwamba, Kanisa linawatumainia katika kushuhudia uzuri wa upendo wa Mungu unaowasaidia watu kutambua kwamba, kweli wanapendwa sana na Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kuwa mashuhuda kwa kuwajali jirani zao, hasa wale wanaotengwa, waliojeruhiwa na kubezwa katika jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.