Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Mwendelezo wa sala na kufunga kwa ajili ya amani duniani!

Papa Francisko pamoja na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Vatican baada ya kuhitimisha mafungo yao kama sehemu ya maandalizi ya adhimisho la Fumbo la Pasaka, wameendelea pia kusali na kufunga kwa ajili ya kuombea amani duniani.

24/02/2018 08:16

Baba Mtakatifu Francisko na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Vatican, Ijumaa, tarehe 23 Februari 2018 wamehitimisha mafungo yao ya Kwaresima kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Mafungo haya yameongozwa na Padre Josè Tolentino de Mendonca huko Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma. Mara baada ya mfungo, Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru na kumpongeza sana Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa niaba ya wakleri wenzake waliofaidika na “cheche hizi za maisha ya kiroho”.

Baba Mtakatifu amekaza kusema, sala na mafungo haya yanaendelezwa ili kusali na kuombea amani nchini DRC, Sudan ya Kusini pamoja na Siria. Hizi ni nchi ambazo zinaogelea katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ametenga tarehe 23 Februari 2018 kwa ajili ya kufunga, kusali na kuombea amani sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu amemshukuru Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa kuwasaidia kusikiliza tena na tena kuhusu maisha na utume wa Kanisa. Amewakumbusha umuhimu wa kujizatiti kikamilifu ili kutofifisha maisha na utume wa Kanisa kwa kumezwa na malimwengu au kwa njia ya ukiritimba usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi katika Kanisa la Kristo. Kwa njia ya ushuhuda, rejea na machimbuko mbali mbali anakiri Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Padre Josè Tolentino de Mendonca ni gwiji katika uinjilishaji na utamadunisho wa imani kwa watu anaowafundisha na kufanya nao kazi kama sehemu ya majadiliano ya kidini na kiekumene kwani Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya watu wote. 

Hawa ni watu wanaofanya hija ya maisha ya kiroho huku wakitafuta mambo msingi katika maisha! Baba Mtakatifu anamshukuru Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa kufundisha katika ukweli na uwazi; kwa ujasiri, upole na unyenyekevu wa moyo, mambo ambayo yamewasaidia kuona mwanga mpya katika maisha na utume wao. Amemwomba aendelee kuwakumbuka katika sala na sadaka yake, kwa kutambua kwamba, kama binadamu wanayo madhaifu yao na wametindikiwa neema ya Mungu, kumbe, wanaweza kuanguka dhambini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.

24/02/2018 08:16