2018-02-24 09:09:00

Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha imani na mapendo!


Siku arobaini za kipindi cha Kwaresima zinatuhimiza na kurudia tena na tena mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali, matendo mema na kuwahudumia wahitaji. Haya ni mazoezi ya kiroho yanayoambatana zaidi na kipindi hiki cha kwaresma. Mazoezi haya ya kiroho yanaendana na imani. Yanajengwa juu ya imani, kwa sababu inahitaji imani ili kuyashiriki na hapo hapo yanakuza na kuongeza imani yake anayeyashiriki. Tafakari ya leo, dominika ya pili ya Kwaresima, inatualika tukiangalie kipengele hiki muhimu katika safari yetu ya siku arobaini za Kwaresima ambacho ni kipengele cha imani.

Masomo kwa Ufupi: Somo la kwanza (Mwa. 22, 1-2. 9a. 10-13. 15-18) linaeleza hatua katika maisha ya Abrahamu na katika mahusiano yake na Mungu. Ni mahusiano ambayo bado yalikuwa yanakua. Kama mwanzo wa mahusiano hayo (Mwa. 12,1) ambapo Mungu alimtaka Abraham ayaache mazingira yake yaliyopita na maisha kwa ujumla, hapa anampa jaribu ambalo linaelekea kufuta uzao wa Abraham hapo mbeleni. Hii ni kwa sababu Mungu alimtaka Abraham amtoe sadaka Isaka, mwanae wa pekee ampendaye. Abraham anapokea agizo la Mungu, haulizi ulizi anakwenda mlimani tayari kumtoa sadaka mwanae. Hapo Mungu anatambua imani aliyonayo Abraham , anampa mwanakondoo wa kutoa sadaka na anaongeza ahadi alizokuwa amempa awali. 

Somo la pili (Rum 8, 31b-34) mtume Paulo anawahakikishia waamini wa Rumi kuwa upendo wa Mungu hautowaacha bali utakuwa nao daima. Na anaeleza kuwa sababu ya upendo huo kutokuwaacha ni kwamba tayari Mungu ameshafanya kitu kikubwa sana kwa ajili yao pale ambapo hakumwachilia mwanae wa pekee bali alimtoa afe kwa ajili ya wote.Hii inakuwa ni sababu ya kuimarisha imani ya wakristo wa Rumi ambao walikuwa katika dhiki na mateso yaliyoletwa kwao na dola ya kirumi.

Somo la injili (Mk 9, 2-10) linaeleza tukio la kugeuka sura kwa Yesu mbele ya wafuasi wake watatu ambao ni Petro, Yakobo na Yohane. Katika tukio hili wanatokea Musa na Eliya ambao wanawakilisha Torati na Manabii ambavyo Yesu amekuja kuvikamilisha. Ndani ya wingu linalowatia uvuli inasikika sauti inayosema “huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”. Tukio hili la kugeuka sura kwa Yesu linadokeza utukufu wa Yesu na ufufuko wake atakaoupata baada ya mateso na kifo cha msalabani. Yesu anapowaambia mitume hao wasitangaze kwa sababu huu haukuwa wakati wa kutangaza utukufu wa ufufuko bali ulikuwa ni wakati wa kuwaimarisha. Mitume walihitaji kuimarishwa kiimani ili wanapomwona Yesu anateseka na kufa msalabani watambue kwanza kuwa ameingia katika mateso hayo kwa hiari yake na pia kuwa anatekeleza yaliyokwisha andikwa katika Torati na Manabii kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.

Tafakari: Masomo ya dominika hii ya pili ya kwaresma yanakutana katika dhamira ya imani, “kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo na bayana ya mambo yasiyooneka” (Heb 11,1). Imani hii ni zawadi kutoka kwa Mungu na ni fadhila ya kimungu. Lakini pia inahitaji utashi wa mwanadamu katika kuipokea, kuikuza, kuiishi na kuirithisha kwa wengine. Abrahamu ambaye ni babu yetu wa imani na kielelezo cha imani kwa wote wanaomwamini Mungu anapata sifa hii na kibali toka kwa Mungu kwa sababu tangu alipoianza safari yake ya imani kwa kupokea mwito wa Mungu  ameyasimika maisha yake yote katika imani hiyo. Kwa Abraham imani yake kwa Mungu haikuongoza vipengele kadhaa tu vya maisha yake  bali iliongoza maisha yote. Aliiruhusu imani kuwa jibu na kuwa mwelekeo katika maisha yake yote ya sasa na yajayo. Na ni katika msingi huu aliweza bila kusitasita kuitii sauti ya Mungu na kuwa tayari kumtoa sadaka mwanae Isaka. 

Imani ya Abrahamu ni imani pia iliyozidi kuimarika kadiri alivyozidi kuingia katika mahusiano na Mungu kwa njia ya agano lakini pia kwa njia ya matukio kama hili ambalo lilikuwa pia ni  la kumjaribu.  Ndivyo pia Mtume Paulo alivyokuza na kuimarisha imani ya waamini wa Rumi kwa kuwakumbusha tukio kubwa la upendo wa Mungu katika maisha yao, ukombozi wa Kristo Msalabani. Na ndivyo Kristo mwenyewe alivyopenda kuimarisha imani ya wanafunzi wake kwa kugeuka sura mbele yao mlimani.

Kipindi hiki cha Kwaresima ni kipindi pia cha kuimarisha imani. Mazoezi ya kiroho ambayo Kanisa linaweka mbele yetu ni mazoezi yanayohitaji imani. Bila kuongozwa na imani hawezi mtu kufunga, hawezi kujikatalia, hawezi kufanya toba, hawezi kusali na hawezi kusukumwa kuwasaidia wahitaji. Nje ya imani atapata tu mbadala wa yote haya. Pamoja na mazoezi haya ya kiroho kupata msukumo wake kutoka katika imani, mojawapo ya matunda yake pia ni kuiimarisha imani ya anayeyashiriki. Imani iliyoimarika ni ufunguo wa kulielewa Fumbo la Paska na thamani kubwa ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo katika maissha yetu. Imani iliyoimarika ni nguvu ya kuliishi fumbo hilo la Paska katika maisha.

Padre William Bahitwa.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.