2018-02-23 14:47:00

Ni siku ya sala na kufunga kwa ajili ya kuombea amani duniani!


Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuitenga tarehe 23 Februari, 2018 Ijumaa ya juma la kwanza la kwaresima kuwa ni siku ya kufunga na kusali kwa ajili kuombea amani duniani na kwa namna ya pekee nchi za Sudani ya kusini na DRC, raia wa Jamhuri ya Watu wa Congo waishio Jijini Roma na wajumbe wa kamati kwa ajili ya Sudani ya Kusini wanakusanyika mnamo majira ya saa 11 katika Kanisa la Kuzaliwa Bwana, maeneo ya kiwanja cha Pasquino, ambapo wakongo hukutana husali, watakuwa na saa moja ya kuabudu Ekaristi Takatifu. Baada ya Ibada ya kuabudu, yataanza maandamano ya kimya kimya katika moyo wa sala kuelekea Kanisa la Mt. Marcello ambapo kutakuwa na mkesha wa sala.

Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu anasema, siku hii ya kufunga na kusali kwa ajili ya amani, Kanisa linaonesha ule ukaribu wake wa kimama kwa wale wanaoteseka na kuhitaji msaada wa hali na mali ili kujikwamua kutoka katika maumivu hayo. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kushughulikia kwa ukaribu na kutokomeza kabisa hali ya ghasia na kinzani zinazopelekea madonda, maumivu na vifo vya wanyonge wengi hasa katika nchi za DRC na Sudani ya kusini. Mfano umwagaji wa damu wa hivi karibuni mnamo tarehe 31 Disemba 2017 na tarehe 21 Januari 2018, wakati maandamano ya amani kudai haki zao, wananchi wa DRC waliumizwa vibaya na wengine kuuwawa kwa kushambuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini humo. Bila kusahau wakimbizi wengi wa Sudani ya kusini wanaofariki kwa njaa na ghasia nyinginezo, kiasi cha kuzuia hija ya Baba Mtakatifu nchini humo.

Baba Mtakatifu Francisko kwa ushirikiano wa baadhi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Mashirika kama Caritas Internationalis amekuwa akitoa misaada kwa raia wa nchi hizo ili kupunguza mahangaiko waliyo nayo. Kumbe ni muhimu kila mmoja kuendelea kujiuliza swali “Ni nini naweza kufanya mimi kwa ajili ya amani?”. Kardinali Turkson anasema, inaweza kuwa ni sala, mfungo au sadaka. Lakini pamoja na misaada ya namna hii, ni lazima viongozi wahusika wachukue hatua madhubuti na kuwajibika ili kuhakikisha amani inarejea katika nchi hizi, na kokote duniani.

Kardinali Turkson anawapongeza wana Kanisa nchini DRC, wakiongozwa kwa sauti na ushujaa wa Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, katika harakati za kusimamia kweli na haki, wakitetea wanyonge ili amani iweze kurejea nchini humo. Katika umoja na mshikamano mahususi na Khalifa wa Mtume Petro, Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu linajikita katika kusali na kufunga kwa ajili ya Sudani ya Kusini na DRC, ili Mwenyezi mungu avunjilie mbali kuta za chuki na uhasama, kisha aweke nia njema kwa viongozi wa serikali hizi waweze kutafuta amani kwa njia ya mazumngumzano na salama. Katika mfungo na sala kwa siku hii, waamini wanaalikwa kujiaminisha kwa Mungu kwani Yeye “huwaponya waliopondeka moyo, na kuziganga jeraha zao… huwategemeza wenye upole, na huwaangusha chini wenye jeuri” (Zaburi 147:3;6).

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.