Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Yesu kugeuka sura ni ushuhuda wa utimilifu wa Sheria na Unabii

Tukio la Yesu kung'aa sura mbele ya wafuasi wake ni kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii na hatima yake ni Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! - RV

22/02/2018 16:05

Mpendwa msikilizaji wa Vatican News! Mtume Yakobo anatuambia kwamba “imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo na bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr 11:1). Imani ni tunu ya kimungu ambayo inatufunulia siri za ufalme wa Mungu na kutupatia msukumo wa kushikamana nazo. Yale tunayoyatarajia kutoka kwa Mungu kwa hakika bado hatujayapata. Tunu ya imani inatupatia ujasiri wa kuwa na uvumilivu na kungojea kwa matumaini makubwa. Zaidi ya hayo imani inatuhakikishia uwepo wa yale ambayo macho yetu ya kibinadamu na akili zetu na uelewa wetu wenye ukomo vinashindwa kuufikia au kuutambua. Mfano, tujongeapo kushiriki Ekaristi Takatifu tunachokiona na kukionja katika milango ya kawaida ya fahamu kinapata maana mpya katika mlango wa imani na hivyo kuona kuwa hatuonji mkate au divai bali Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Imani inatuunganisha na Mungu na hivyo katika tunu hiyo utukufu wake unang’aa ndani yake yeye aaminiye. Kristo anatuonesha kile tunachokifikia katika imani. Anapanda juu mlimani na “akiwa katika kusali kwake, sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe yakimetameta”. Dominika iliyopita tulimwona akiwa katika hali hiyo ya sala na kuweza kupambana na vishawishi vya shetani. Muunganiko huu kati ya mwanadamu na Mungu katika imani unachagizwa na tendo adhimu la sala. Sala kama anavyofafanua Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu ni kuinua moyo kwa Mungu. Kitendo hicho kinafafanuliwa na tendo la kupanda mlimani; tendo ambalo linamuondoa mwanadamu katika mwenendo wa kawaida wa maisha na kumkutanisha na Mungu.

Sala ni tendo ambalo linayaweka mawazo ya Mungu katika mstari wa mbele hata pale yanapoonekana kukinzana na mazoea au matakwa ya kibinadamu. Baba yetu wa imani Ibrahimu anatuonesha maana hiyo ya sala kwa matendo. Pamoja na kwamba aliahidiwa kuwa baba wa mataifa mengi (Rej Mw 17) na pia akapewa mtoto katika uzee wake, lakini anapoagizwa na Mungu amtoe sadaka yeye hakusita kwa sababu aliishi sala kivitendo. Maisha yake ya imani yalimuungnisha na Mungu wakati wote na kumwezesha kuyaona na kuyaelewa mawazo yake kadiri alivyotaka Mungu. Utukufu wa Mungu daima uling’aa ndani mwake na yeye alitafuta kumwadhimisha kwa maisha yake yote.

Mtume Petro na mitume wenzake waliweza kuuona utukufu wa Mungu kwa kitendo hicho cha kupanda mlimani. Hili ni dokezo kwetu kwa kipindi hiki cha Kwaresima, kipindi cha neema ambacho kinamwalika kila mmoja kupanda pamoja na Kristo, juu mlimani kwa makusudi ya kuuona utukufu wa Mungu. Kilele cha majira haya ni Sherehe ya Ufufuko wa Kristo ambayo ni utimilifu na uthibitisho wa imani yetu. Mitume walipokuwa wanashuka walionywa kutokueleza watu juu ya utukufu waliouona hadi wakati wa Ufufuko. Maana yake ni nini katazo hilo? Ni pedagogia ya kimungu ambayo ilinuia kuwapitisha Mitume katika safari nzima ya ukombozi hadi kashfa au makwazo ya msalaba; pedagogia ambayo ilinuia kuwasambaratisha kwa muda na kuwakatisha tamaa lakini baadaye kutiwa nguvu kwa fumbo la ufufuko wa Kristo. Kristo alinuia kuwafanya wawe na utulivu ili kuiona maana ya utukufu huo wanaouona kuwa kweli ni haiba yake hata kama atapitia katika njia ambayo kibinadamu inaweza kuchukuliwa kuwa ni aibu na fedheha.

Sauti kutoka mbinguni ilisikika ikisema: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye”. Baada ya agizo hilo tunaambiwa kwamba “hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake”. Uwepo wa Mungu na utukufu wake ulipong’aa katika Kristo walionekana pamoja naye Musa na Eliya ambao waliiwakiisha Torati yote na Manabii. Uwepo huu ulimfadhaisha Petro na mitume wenzake kiasi cha kutaka kuwajengea makao, ishara ya uendelevu wa uwepo wa utukufu wa Mungu milele. Lakini agizo kutoka mbinguni na uwepo wa Kristo peke yake baada ya agizo hilo unatuonesha moja kwa moja ujumuisho wa Torati yote na Manabii katika nafsi ya Kristo. Utukufu huo, yaani uwepo wa Mungu unajithibitisha katika Kristo ambaye ni Mwana wake; Yeye ambaye ni nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu sana anakuwa kwetu ufunuo wa utukufu wa Mungu. Imani yetu katika Neno lake ndiyo hakika ya uwepo wa Mungu kati yetu.

Majira ya Kwaresima ni fursa ya kuuonja tena upendo huu mkubwa wa Mungu. Pamoja na kwamba mwanadamu anaangukia dhambini mara kwa mara lakini ametuwekea Kristo kuwa kati yetu kama Yeye anayetuombea. Hivyo imani yetu kwake inapaswa kukolezwa ili kuikwepa hukumu yake na kuipokea haki yake au kuikwepa adhabu yake na kuikumbatia huruma yake. Mtume Paulo anatuhakikishia kwa maneno yake akisema: “Mungu akiwepo upande wetu, ni nani aliyeko juu yetu?”. Mzaburi anatuonesha namna nyingine njema ya kuuona utukufu wa Mungu katika hali ya imani. Hii ni katika juhudi za kuwa hai kiroho. Yeye anasema: “Nitaenenda mbele za Bwana katika nchi za walio hai”. Uhai huo wa kimungu unamwezesha kupita katika mzingira magumu. Ingawa anaweza kuonekana kufa mbele ya macho ya watu lakini yeye anaimba kwa furaha na ujasiri akisema: “ina thamani machoni pa Bwana, mauti ya wacha Mungu wake”.

Leo hii tunaishi katika jamii ambayo inapaswa kuwa na kiu ya pekee ya uwepo wa Mungu. Jamii ya mwanadamu imepoteza hamu na hisia za uwepo na Mungu na matokeo yake ni kuishi katika kizazi ambacho kimelowea katika maisha ya dhambi. Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili katika mausia yake ya kitume Reconciliatio et Paenitentia, alisema yafuatayo: “Dhambi, kama mpasuko wa uhusiano na Mungu, ni kitendo cha kutotii kinachofanywa na kiumbe ambaye humkataa Yeye ambaye kwake ametoka na ambaye anayawezesha maisha yake. Hivyo ni kitendo cha kujiua” (Rejea Reconciliatio et Paenitentia, namba 15). Hivyo dhambi inatajwa kama tendo ovu ambalo linaipora hadhi ya utukufu ndani mwetu kwani mwanadamu kwa uhuru wake anaukataa uwepo wake na kutupilia mbali uwepo wake unaomfadhili kila siku.

Dhambi inaondoa imani yetu kwa Mungu na hivyo kufifisha utukufu wake katikati yetu. Na hivyo, anaendelea Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kutuambia: “Kwa kuwa kwa kutenda dhambi mwanadamu anakataa kujikabidhisha kwa Mungu, uwiano wake wa ndani unaharibiwa na kwa hakika ni ndani mwake ukinzani na magombano hayo hutokea. Anapojeruhiwa namna hii, mwanadamu anakuwa ameuharibu kabisa mfumo wa mahusiano yake na wengine na uumbaji wote”. Hapa tunaona ukosefu wa imani unavyoweza kuharibu utukufu wa Mungu si kwa mwanadamu tu bali kwa ulimwengu mzima. Maovu mbalimbali ya dunia ni matokeo ya kupotea utukufu huo wa Mungu kunakosababishwa na kupotea kwa imani katikati ya wanadamu. Tukitumie kipindi hiki mahsusi kwa ajili ya kuinoa na kuimarisha imani kusudi uwepo wa Mungu uendelee kuwepo katikati yetu na utukufu wake unaofunuliwa kwetu kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo uendelee kutung’aria katika maisha yetu!

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.

Vatican News!

22/02/2018 16:05