Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Ng'oeni ndago za ukabila uchwara unaopandikiza mbegu ya kifo!

Familia ya Mungu nchini Ethiopia imetakiwa kung'oa ndago za ukabila zinazopandikiza utamaduni wa kifo. - REUTERS

22/02/2018 15:38

Kardinali Berhaneyesus D. Souraphiel, Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA, katika tamko lake kwa waandishi wa habari hivi karibuni, anasikitika kusema, Ethiopia ambayo ilikuwa imeanza kujivunia kwa kasi kubwa ya ustawi na maendeleo imejikuta ikitumbukia katika kinzani na migogoro inayopelekea umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na uharibifu wa mali ya watu. Vitendo hivi ni kikwazo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya wengi. Kutokana na changamoto hii, viongozi mbali mbali wa kidini wameamua kuingilia kati mgogoro huu ili kuhakikisha  kwamba, Ethiopia inarejea tena katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wake.

Wananchi watambue kwamba, wote ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu na kamwe, ukabila na udini usiokuwa na mvuto wala mashiko visiwe ni sababu ya kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii nchini Ethiopia, kwani, hii si sehemu ya utamaduni wa wananchi wa Ethiopia. Kila mtu aliyezaliwa nchini Ethiopia ni mwananchi wa Ethiopia ana haki na utu sawa na kwamba, ni sehemu ya mapokeo ya Ethiopia. Wananchi wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Utamaduni wa kifo ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Ukabila ni hatari sana kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya wananchi wa Ethiopia kwani hautawaacha salama kwani chuki na uhasama vitaendelea kurithishwa kizazi baada ya kizazi. Huu si urithi ambao familia ya Mungu nchini Ethiopia inapaswa kuwaachia watoto na wajuu zao. Watoto warithishwe: umoja, upendo, udugu na mshikamano na wala si chuki na mipasuko ya kijamii na ukabila ambao kimsingi ni sumu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu na heshima ya wananchi wa Ethiopia vinapaswa kulindwa na kudumishwa. Ethiopia ina heshima kubwa sana ndani na nje ya Bara la Afrika kwani hapa ni makao makuu ya Umoja wa Afrika na kuna zaidi ya mabalozi 330 wanaoishi na kufanya shughuli zao nchini humo.

Kardinali Berhaneyesus D. Souraphiel, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali, ili kuombea: haki, amani na maridhiano kati yao hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, ili kurejesha tena utu na heshima kwa kila mwananchi. Viongozi wa Makanisa nchini Ethiopia wanasikitishwa sana na uamuzi wa uchungu uliochukuliwa na Bwana Hailemariam Desalegn, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia aliyeamua kung’atuka kutoka madarakani, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya nchi ya Ethiopia, ikiwa kama yeye alidhaniwa kuwa ni kikwazo katika mchakato huu. Waziri mkuu mpya atakayeteuliwa atambue changamoto kubwa iliyoko mbele yake katika ujenzi wa taifa la Ethiopia. Wananchi wawe wazi, wakweli na waaminifu kutoa na kushirikisha mawazo yao ili kusaidia ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano nchini Ethiopia. Tarehe 26 Februari 2018, Kanisa nchini Ethiopia litafanya kumbu kumbu ya Mashujaa wa Ethiopia, watu waliojisadaka kwa ajili ya kutetea uhuru wa nchi yao bila kumezwa na “ukabila uchwara” wakashikamana na kujenga umoja wa kitaifa. Siku hii iadhimishwe kwa sala na kufunga kwa ajili ya kuombea haki, amani na maridhiano nchini Ethiopia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

22/02/2018 15:38