Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki DRC: Uhuru, Usalama & Demokrasia

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka Serikali iliyoko madarakani kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa na uhuru wa kujieleza, wanapatiwa ulinzi na usalama wa maisha na mali zao pamoja na kuwa na demokrasia inayozingatia utawala wa sheria. - REUTERS

21/02/2018 07:20

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema: kufunga na kusali; kuchunguza dhamiri zao, ili hatimaye, kuweza kusikiliza kilio cha mateso na mahangaiko ya wananchi wa DRC na Sudan ya Kusini. Anawataka wajiulize swali la msingi, Je, wao wanaweza kufanya nini ili kudumisha amani na utulivu! Jibu la kwanza kwa hakika anasema Baba Mtakatifu, ni kusali na kila mmoja kujizatiti kuachana kabisa na vitendo vinavyochochea: vita, ghasia na mipasuko ya kijamii. Hii inatokana na ukweli kwamba, ushindi unaopatikana kwa njia vita na ghasia ni ushindi batili, lakini kushikamana kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani, ni msaada mkubwa, kikolezo kikuu cha maendeleo na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu kwa kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini na DRC, ameitisha tarehe 23 Februari 2018 kuwa ni siku maalum kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani! Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, daima anasikiliza kilio cha watoto wake, wanaomkimbilia kwa machozi na mateso makubwa wakiomba msaada wake, ili kuwaponya waliopondeka moyo na kuziganga jeraha zao.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, kuanzia tarehe 15 – 17 Februari 2018 limefanya mkutano wa dharura uliojadili pamoja na mambo mengine hali ya kisiasa na kijamii nchini humo hasa kutokana na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia. Maaskofu wanakaza kusema, Kanisa halina chama cha kisiasa, bali waamini wake wana vyama vyao wanavyovishiriki kama sehemu ya utekelezaji wa haki yao msingi kidemokrasia. Kanisa linataka kusimama kidete, kulinda, kutetea: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa DRC. Kanisa linapinga utamaduni wa kifo unaosababishwa na mateso pamoja na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, hali ya kiuchumi na kijamii nchini humo inaendelea kudidimia kila kukicha! Utawala wa sheria umewekwa rehani na sasa vyombo vya ulinzi na usalama vinatumika kwa ajili ya kuwatesa na kuwanyanyasa wananchi wasiokuwa na hatia na matokeo yake ni umwagaji wa damu. Maaskofu wanasikitishwa sana na wimbi la mashambulizi ya Serikali yanayoelekezwa dhidi ya Kanisa, taasisi na viongozi wake, kiasi hata cha kutishia usalama na maisha ya Kardinali Laurent Pasinya Monsengwo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa.

Maeneo mengi nchini humo, hayana uhakika wa usalama wa maisha ya wananchi wengi, kiasi hata cha kuhatarisha mchakato mzima wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2018. Maaskofu wanakaza kusema, bila haki, amani na usalama ndoto za uchaguzi huru na wa haki zitafutika mara moja kama “ndoto ya mchana” na matokeo yake ni kuendelea kuitumbukiza nchi katika maafa kutokana na uchu wa mali na madaraka. Maaskofu wanaitaka familia ya Mungu nchini DRC kusimama kidete kupinga kwa nguvu zote mambo yote yanayotishia: usalama, ustawi, maendeleo, umoja na mshikamano wa kitaifa. Wananchi waendelee kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliopoteza maisha yao kwa kudai haki msingi za wananchi wa DRC. Waendelee kuonesha mshikamano na waathirika wa vitendo hivi kwa hali na mali.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC limetoa mapendekezo kadhaa ili kuhakikisha kwamba, haki, amani, demokrasia na utawala wa sheria vinarejeshwa na kushika mkondo wake. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, makubaliano ya amani kati ya Serikali na vyama vya upinzani yaliyotiwa mkwaju kunako tarehe 31 Desemba 2016 yanatekelezwa kikamilifu, ili kuweza kufanya uchaguzi huru na wa haki hapo tarehe 23 Desemba 2018. Hali ya kisiasa nchini DRC inapaswa kuboreshwa zaidi ili kuondokana na hofu iliyotanda kwa wakati huu miongoni mwa wananchi. Wananchi waruhusiwe kufanya maandamano ya amani. Wahusika wote waliosababisha vurugu, ghasia na mauaji sheria ichukue mkondo wake. Ulinzi na usalama vizingatiwe pale ambapo wananchi wanapo tekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa kudai uchaguzi nchini humo, kama inavyofanyika sehemu mbali mbali za dunia, ili kuunga mkono jitihada za wapenda amani kutaka kurejesha tena: haki, amani na maridhiano nchini DRC. Serikali iache vitisho na mashambulizi dhidi ya waandamanaji kwani kufanya hivi ni kwenda kinyume kabisa cha Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni Sheria mama.

Maaskofu wanasema kwamba, DRC inahitaji uongozi makini utakaosaidia kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, demokrasia, umoja na mshikamano wa kitaifa. Uongozi utakaokuwa tayari kulinda na kusimamia mipaka ya nchi pamoja na usalama wa raia na mali zao. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia katika harakati za utekelezaji wa mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wakati huo huo, tarehe 9 Februari 2018 kumeadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia katika kipindi cha mwezi Desemba 2017 na Januari 2018 wakipigania haki, amani na demokrasia ya kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

21/02/2018 07:20