2018-02-21 16:00:00

Kristo Yesu anawaandaa wafuasi ili kulikabili Fumbo la Msalaba!


Katika makanisa ya Bizantini huko Ulaya Mashariki, sura ya Kristo huoneshwa kama Bwana na Mtawala wa muda na wakati wote. Ndiyo tafakari yetu ya leo – sura kamili ya Kristo inawekwa mbele yetu.  Sote twajua kuwa maisha ya Kristo ni fumbo. Lakini yeye ametuonesha Mungu na hivyo twaweza kuongea juu ya utukufu wa Mungu ulioonekana kwetu. Hali hii yatuonesha kuwa Yesu alijionesha kwetu na hivyo hakubaki tu fumbo. Sikia sauti ya Mungu “huyu ndiye mwanangu mpendwa wangu msikilizeni yeye”. Hilo fumbo limefunuliwa kwetu. Kwa tamko hili urithi wetu kama wana wa Mungu unawekwa wazi. Leo Mungu ajionesha kwetu.

Mt. Yohane wa Msalaba anasema – tangu Baba alipotamka pale mlimani Tabor – huyu ndiye mwanangu mpemdwa msikilizeni yeye, Mungu Baba kwa namna moja, alikamilisha ufunuo wake, akabaki bubu. Alisema kila kitu. Hana kitu kingine kipya cha kufunua. Alikamilisha ufunuo wake kwetu. Alama zilizopo: a. Mlima - mahali pa agano kati ya Mungu na mtu – sasa yaonekana wazi kuwa mlima mpya wa Mungu ni Yesu – Yesu ni mahali pa kukutana kati ya Mungu na watu – siyo tena mlimani. B. Mawingu na kivuli – yaonesha uwepo wa Mungu – mjumbe sasa ni Kristo. C. Sauti ya Mungu; huyu ndiye mwanangu – Mungu anajifunua kwetu, na kusema yeye ni nani - sasa tuna dunia mpya, namna mpya ya kuelewa ukweli, namna mpya ya kuishi, namna mpya ya kuishi imani yetu na namna mpya ya kuishi maisha yetu – pamoja na Kristo tunao ufahamu mkubwa kuhusu Mungu. Yesu ndiye sheria mpya, ni juu zaidi ya sheria za mwanadamu na manabii.

Kugeuka sura – ni utangulizi wa Pasaka – tunapoitwa sisi sote katika ushuhuda wa imani yetu ya kila siku – hivyo maisha yetu yahitaji ufunuo wa Mungu hata katika maisha ya kawaida.  Kugeuka sura – huangaza matembezi yetu ya imani- mitume waliona utukufu wa Mungu. kwa maisha yetu ya kila siku – wengine wanaweza kuuona utukufu wa Mungu? Kugeuka sura – huangaza pia maisha yetu ya zamani – mazuri na mabaya – yale mazuri yanaendelezwa na mabaya yanaachwa. Neno la Mungu siku hii ya leo – lazima lituvuruge katika imani yetu – kile kilichodhaniwa kuwa fumbo sasa si fumbo tena kwa maana ya kuwa Mungu yu pamoja nasi na ameonekana kwetu na ametuambia wazi kile tutakiwacho kufanya – kugeuka sura. Hakika imani yahitaji kusaidiwa na matokeo hai – leo tunapata bahati hiyo. Ni msukumo na changamoto kwetu sisi kuishi kama watu wa mwanga  na si wa giza tena. Tumgeukie Mungu mwanga wa kweli ili atuangaze, atuongoze na kugeuza mioyo yetu.

Katika ujumbe wa Kwaresima uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kunako mwaka 2015 kwa kuongoza na kauli mbiu “ZINGATIENI HAKI NA KUTENDA MEMA” (Rej. Isa. 56:1) tunaambiwa kuwa kwaresima ni kipindi cha toba na uongofu wa nafsi zetu – tujiandae kuruhusu nafsi zetu zitajirishwe kwa neema ya Mungu ya ufufuko. Katika kipindi cha kwaresima, imani inaimarishwa, matumaini ya kweli yanafufuliwa, upendo ulioanza kuchakaa unasafishwa na Pasaka ya milele inaandaliwa. Hiki ni kipindi ambacho kanisa, kupitia Neno la Mungu na mazoezi ya kiroho, linatukumbusha na kutuelekeza kurudi na kulielekea lengo la juu kabisa la maisha yetu katika uhusiano mkamilifu na Mungu. Ukamilifu wa uhusiano na Mungu, ambao kwao uhusiano wote wa biandamu unaratibiwa, unajengwa juu ya msingi wa wema na haki. Je, nasi tumegeuka sura zetu au tumebaki hivyo hata baada ya kukutana na Mungu?

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. Reginald Mrosso, c.pp.s.








All the contents on this site are copyrighted ©.