Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan: Fungeni na kusali kuombea amani

Maaskofu Katoliki Sudan: Fungeni na kusali ili kuombea haki, amani na upatanisho wa kitaifa! - AFP

21/02/2018 11:52

Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan linamshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameendelea kuwa na jicho la pekee sana kwa mateso na mahangaiko ya maskini sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee kwa familia ya Mungu, Sudan ya Kusini. Maaskofu wanaitikia kwa mikono miwili wito wa Baba Mtakatifu wa kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini humo na DRC, maeneo ambayo kwa sasa hayana matumaini sana, lakini nguvu ya kufunga na kusali inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu.

Askofu Barani Eduardo Hiiboro Kussala, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan anasema, amani na utulivu ni muhimu sana Kusini mwa Sudan ambayo kwa sasa inaogelea katika maafa makubwa ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kutokana na uchu wa mali, madaraka na ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu anaendelea kujipambanua sehemu mbali mbali za dunia kama chombo na shuhuda wa amani. Ameendelea kutoa matumaini kwa familia ya Mungu Sudan ya Kusini na kwamba, Kanisa lina matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu atasikiliza sala na kilio chao na kuwa iko siku ataganga na kufunga majeraha ya mioyo iliyovunjika na kupondeka huko Sudan ya Kusini, mchakato unaofumbatwa katika uponyaji, upatanisho na ujenzi wa umoja wa kitaifa. Kipindi cha Kwaresima ni muda muafaka wa toba na wongofu wa ndani; kipindi kilichokubalika cha upatanisho kati ya waamini na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao.

Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa uwepo na mshikamano na watu wao. Askofu Barani Eduardo Hiiboro Kussala anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kurejea tena na tena katika ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2018. Baba Mtakatifu anaonya kuhusu uwepo wa manabii wa uongo; mioyo migumu na baridi. Kanisa ambalo ni Mama na Mwalimu katika Kipindi cha Kwaresima linatoa dawa ya ukweli hata kama ni mchungu kiasi gani kwa kuwataka watoto wake kujikita katika sala, kufunga na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kuonja huruma na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayewatakia maisha bora zaidi.

Sudan ya Kusini inahitaji kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kutoa fursa kwa wananchi wote kufurahia uhuru na hatimaye kuonja huruma na upendo katika maisha yao. Watambue kwamba, wote ni sehemu ya familia ya Mungu, kumbe, wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; uchoyo na ubinafsi mambo yanayokwamisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na mapendo kwa kudumisha Injili ya amani, haki na maridhiano.

Ili kuweza kufikia hatua hii, kuna haja kwanza kabisa ya watu: kusamehe na kusahau; kwa kujikita katika ukweli na uwazi; toba, wongofu na msamaha wa kweli; ili kuganga na kuponya; kusamehe na kusahau tayari kujenga amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Kwaresima ya Mwaka 2018 kiwe ni kipindi cha: toba na wongofu wa ndani; sala na ibada; matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha mshikamano wa upendo. Kufunga kusaidie kurekebisha vilema na udhaifu wa binadamu, ili kuondokana na ghasia pamoja na vurugu sanjari na kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika huduma makini kama sehemu ya maandalizi ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana. Kwaresima ni muda muafaka wa kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: Ukweli, Haki na Amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

21/02/2018 11:52