2018-02-20 14:30:00

Ukame wa maisha ya kiroho na changamoto zake!


Ukame wa maisha ya kiroho ni kati ya changamoto zinazowakabili waamini wengi kiasi hata cha kukosa kipimo sahihi cha kuweza kufanya tathmini ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Jambo la msingi ni waamini kuhakikisha kwamba, wanazama katika undani wa maisha yao, ili kugundua ukame unaowatesa, ili hatimaye, kuupatia dawa madhubuti inayojikita katika imani, kwa kutambua udhaifu na mapungufu yanayowakabili katika uhalisia wa maisha yao bila kujionea aibu. Padre Josè Tolentino de Mendonca katika tafakari yake ya tatu kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumatatu, jioni, tarehe 19 Februari 2018, amekazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa kutambua kiu na njaa inayomsonga mwamini katika maisha yake; kutafuta vigezo mahususi ili kupima kiu na njaa hii ya maisha ya kiroho, tayari kuipatia tafsiri makini katika maisha, kwa kutambua kwamba, kiu na njaa ya kweli ni kuuona Uso wa Mwenyezi Mungu.

Kwa njia hii, waamini pia wataweza kutambua utajiri uliomo ndani mwao, tayari kuufanyia kazi kwa nia njema, ili hatimaye, uweze kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha kama anavyo kaza kusema Mwanataalimungu mahiri Bemard Lonegran. Waamini wajenge utamaduni wa kujichunguza, kujifahamu, kujikubali na hatimaye kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu anayewatambua jinsi walivyo. Mchakato huu ni kielelezo cha ukomavu wa maisha ya mwamini, unaoweza kumpatia nguvu ya kupiga moyo konde kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu na kukimbilia tena huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu unaowarejeshea tena: imani, matumaini na mapendo kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu!

Mwenyezi Mungu anawapenda watoto wake jinsi walivyo, anawapatia nafasi ya kutubu na kumwongokea, ili waweze kuwa ni watu wema zaidi. Waamini katika hija ya maisha yao, wajitahidi kutambua kiu na njaa inayowasumbua katika maisha ya kiroho ili kuipatia tiba muafaka itakayowasaidia kuendelea kuwa waaminifu na watu wakweli katika maisha. Kwa njia ya neema wataweza kugundua ndani wao makovu ya dhambi, upweke, mnachungu ya moyo na kiu ya kutaka kukombolewa. Maisha ya kiroho yanafumbatwa katika uhalisia wa watu wenye utambulisho wao.

Ikumbukwe kwamba, kiu na njaa ya maisha ya kiroho: vinagusa undani wa mtu wakati wa raha, shida, magumu pamoja na furaha. Upyaisho wa maisha ni mchakato endelevu ili kuzima kiu ya maisha ya uzima wa milele na matamanio halali ya binadamu. Kwa mwelekeo huu, Kanisa linakuwa ni Sakramenti ya wokovu; chombo cha mawasiliano kati ya binadamu na Mwenyezi Mungu. Waamini wajenge tabia na utamaduni wa kusikiliza kwa dhati kiu na njaa ya maisha ya kiroho inayofumbatwa katika ukweli; wema, uzuri na upendo.

Padre Josè Tolentino de Mendonca anasema, waamini wajifunze kuratibu vionjo na matamanio yao halali, tayari kumkaribisha Mwenyezi Mungu anayebisha hodi katika maisha ya waamini wake. Watu wanapenda kuangaliwa, kulindwa, kuaminiwa pamoja na kujikita katika imani. Watu wana kiu ya kupenda na kupendwa; kutambuliwa na kuthaminiwa uwepo wao. Watu wajifunze kuwa wazi na wa kweli mbele ya jirani zao, Jambo la kujiuliza ni ikiwa kama waamini wanajenga Jumuiya inayotamaniwa na wengi kwa kutambua kwamba, Kanisa ni maabara inayowawezesha vijana kutoa unabii; wazee kuwa na ndoto na vijana wanao upeo mpana zaidi wa mambo mbali mbali!

Haya ni mambo ambayo pia yanagusa masuala ya kitamaduni, kiuchumi na kisayansi. Kanisa lina kiu ya haki inayopaswa kutekelezwa mintarafu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” ili kuweza kulipyaisha Kanisa kwa njia ya uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, utamadunisho ili Injili iweze kugusa mila na desturi za watu sanjari na kukuza ari na utume wa kimisionari kwa watu mbali mbali!

Yote haya anasema Padre Josè Tolentino de Mendonca, ni kwa ajili ya kuliwezesha Kanisa kuzima kiu ya uwepo wa Mungu kwa waja wake; upendo unaojidhihirisha pia hata katika kazi ya uumbaji. Katika shida na mahangaiko mbali mbali, watu wanakuwa na shauku ya kutaka kuuona Uso wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli walipokuwa uhamishoni. Kiu ya kuuona Uso wa Mungu inakuwa kali kiasi hata cha kugeuka kuwa kama sala endelevu. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kugundua tena ndani mwao kiu na hamu ya kutaka ya kuuona Uso wa Mungu, ili aweze kuwagusa tena katika undani wa maisha yao kama alivyofanya Yesu kwa kumponya mgonjwa wa ukoma kwa kumgusa; alivyomponya mkwewe Petro; mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka 12; vipofu pamoja na wagonjwa mbali mbali! Hata mitume waliguswa na Kristo wakati ule alipogeuka sura, ili kuwaandaa kikamilifu kukabiliana na Fumbo la Pasaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.