2018-02-20 14:52:00

Madhara ya utupu wa maisha ya kiroho!


Kiu inayofumbatwa katika utupu ni hatari katika maisha ya mwamini; pale mtu anaposikia moto ukiwaka ndani mwake, anaweza kuchanganyikwa na hivyo kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Hali ya namna hii inahitaji kupewa tiba muafaka ili kukata kiu ya matamanio yasiyo halali katika maisha ya mwamini. Waamini watambue ndani mwao uhuru unaoweza kuwaletea huzuni katika maisha, daima wakiwa tayari kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu! Haya ndiyo yaliyojiri katika tafakari ya Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumanne asubuhi, tarehe 20 Februari 2018.

Kiu ya kweli inamfanya mwamini kutafuta na kujifunza; kushirikiana na kushikamana na wengine, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani pamoja na kubadilishana mawazo na changamoto za maisha. Utupu katika maisha unafumbatwa katika ubaridi wa moyo kiasi cha kuvuruga mahusiano ya kijamii na hatimaye, kukosa mwelekeo sahihi wa maisha unaosababisha dharau, hasira, chuki na kinzani kiasi hata cha mtu kujisikia kuwa ametelekezwa katika maisha. Ufinyu na mawazo mgando ni mambo yanayoweza kumtumbukiza mtu katika upweke hasi kwa kukosa: imani na ukweli wa maisha.

Utupu huu unajionesha kwa watu kumezwa na malimwengu na hivyo kukosa matumaini na mvuto kwa watu! Huu ni ugonjwa unaopaswa kupatia tiba muafaka kwani hii ni kiu ya utupu wa maisha. Hali ya kukata tamaa na kukosa maana ya maisha na utume wa Kanisa ni mambo yanayoweza kuwakumba hata viongozi wa Kanisa katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao. Hawa ni watu wasioridhika na mafanikio wanayopata; wanahisi kunyanyaswa na kuonewa na wakubwa; matokeo yake wanakuwa kama watu wa mshahara. Hali hii inawakumba hasa mapadre vijana kati ya umri wa miaka 25 - 29 na wazee wenye umri zaidi ya miaka 70. Hizi ni dalili za ukosefu wa maboresho ya maisha ya kiroho na msongo wa mawazo ambao kimsingi unahitaji mapumziko ya kutosha. Inasikitisha kuona kwamba, hakuna upendo na mshikamano miongoni mwa wakleri; wala mafungamano wakati wa raha na shida; ni watu ambao wamejifunza mengi, lakini kwa bahati mbaya hawana sanaa ya kusikilizana wala kupendana!

Maisha ya kijumuiya yanakuwa ni mzigo mzito sana usioweza kubebeka. Hizi ni dalili za utupu wa maisha na matokeo yake ni kuanza kumezwa na malimwengu, ulevi wa kupindukia au matumizi haramu ya njia za mawasiliano ya kijamii. Maisha ya binadamu yanaendelea kubaki kuwa ni fumbo ambalo kuna baadhi ya watu wamejeruhiwa sana katika maisha yao; wametikiswa na umaskini au vita. Kila mtu katika maisha ana uzuri na mapungufu yake. Jambo la msingi ni kwa kila mtu kukubali jinsi alivyo na kuanza mchakato wa mabadiliko na upyaisho wa maisha kadiri ya mwanga wa tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Hapa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuisikiliza sauti ya Mungu inayozungumza nao kutoka katika dhamiri nyofu, kwa kujiweka wazi mbele ya Mungu, ili kuonja huruma na upendo wake badala ya kukimbia na kujificha kama alivyofanya Nabii Yona. Lakini Yakobo alipambana na hali yake hadi akafanikiwa kupata baraka ya Mungu na kwenda kuhubiri toba na wongofu wa ndani kwa wananchi wa Ninawi alionja tena huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Padre Josè Tolentino de Mendonca anafafanua kwamba, uhuru wa huzuni kadiri ya Maandiko Matakatifu ulishuhudiwa na yule kijana tajiri anasimuliwa kwenye Injili ya Mathayo na Marko. Huyu ni kijana aliyetaka kuanzisha urafiki na Kristo Yesu, akamwonesha matumaini na Yesu akampenda. Lakini alipoambiwa kwenda kuuza mali zake zote kisha kumfuasa Kristo Yesu akashikwa na huzuni kubwa kwa sababu alikuwa na mali nyingi ambayo kimsingi ilimnyima ile furaha ya kweli na hivyo kumtumbukiza mtu katika ugonjwa. Waamini wajifunze mapambano ya maisha ya kiroho, daima wakiwa tayari kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu, huku wakichukua vyema Misalaba ya maisha yao na kufuata nyayo za Kristo. Watambue kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali. Yesu mwenyewe anasema, njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.