2018-02-20 07:24:00

Italia wekezeni katika elimu na afya na wala si silaha huko Niger!


Wamisionari wa Italia wanaofanya utume wao nchini Niger, wanatazama kwa mashaka sana mpango wa Italia kutuma vikosi vya kijeshi nchini Niger kwa madai ya kusimamia haki na utulivu nchini humo. Kwa mujibu wa wamisionari hao, wanaona mpango huo una lengo la kuwanyonya wananchi wa Niger. Padre Vito Girotto wa Jumuiya ya Maisha ya  Kitume ya Wamisionari wa Afrika, katika mahojiano na Sir da Niamey anasema, katika hili Italia inatumika kama kibonyezeo cha mbali, remote ya control cha nchi ya Ufaransa, na ni hii ishara wazi ya ukoloni mamboleo.

Niger ingawa inatambulika kuwa moja ya nchi maskini sana duniani, ni nchi yenye utajiri mwingi wa Uranium, Mafuta ya Petrol na Dhahabu. Serikali ya Italia inaonekana kuwa na matamanio ya maliasili hizo, na wakati huo huo wafaransa ambao wanashutumiwa kupelekea umaskini wa nchi hiyo, kwa raia wa Niger, wanatambulika bado kama wakoloni; na inaonekana wanafanya urafiki na serikali ya Italia ili kuendelea kuwanyonya na kuwaonea wananchi wa Niger. Huu ni ukoloni mamboleo, anasema Padre Vito Girotto.

Kadiri ya Padre Vito Girotto, unapoongelea majeshi unaoongelea silaha, na silaha zinaleta woga. Tendo la kupeleka vikosi vya kijeshi nchini humo, litaongeza hasira ya vijana wa nchi ya Niger, ambapo takwimu zinaonesha zaidi ya nusu ya raia wa nchi hiyo wana umri chini ya miaka 18. Kama kweli nia ni kuwasaidia wananchi wa Niger, ingekuwa vema kuwekeza kwenye elimu na masuala mengine ya maendeleo kuliko kupeleka vikosi vya kijeshi. Gharama za vikosi hivyo kwa mwaka 2018 ni makadirio ya Euro 49.5 milioni, ambazo zingeweza kuwekezwa katika maendeleo badala ya kusafirisha vikosi vya kijeshi, jambo ambalo linaweza kupelekea hatari ya migomo na ghasia kutoka kwa vijana wa Niger. Nchini Niger wakatoliki ni kundi dogo ambalo ni takribani ya waamini 50,000 tu, na wanahudumiwa na wamisionari 7 kutoka Italia: 4 ni wa Jumuiya ya Maisha ya Kitume ya Wamisionari wa Afrika; 3 ni Zawadi ya Imani, fidei donum, kutoka majimbo ya Lodi na Milan. Wamisionari wote hawa wanapinga mpango wa Italia kupeleka vikosi vya kijeshi nchini Niger, na wanadai ni aibu kwa waitalia.

Na Padre Celestine Nyanda.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.