2018-02-20 06:43:00

Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo: tiba ni toba na wongofu!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kujizatiti, kuwajibika pamoja na kuonesha utashi wa kisiasa katika kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, ili kuondokana kabisa na janga hili linaloathiri utu, heshima na haki msingi za binadamu!  Kuwakamata na kuwashughulikia wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni tendo la haki, lakini suluhu ya kudumu ni toba na wongofu wa ndani, ili kuachana kabisa ya tabia hii chafu inayopandikiza utamaduni wa kifo! Maafisa wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama, maaskofu, watawa wa kike na wa kiume, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kutoka kona zote duniani, tarehe 8 – 9 Februari 2018 walikusanyika mjini Vatican kwa ajili ya mkutano wa tano wa kikundi cha Mtakatifu Martha kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, ambapo wamepeana mrejesho na kushirikishana utendaji wao katika harakati za kutokomeza janga hilo.

Mkutano wa mwaka huu umelenga kushirkishana uhalisia na utendaji wa kikanda, changamoto na mafanikio, katika kupiga vita biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo katika mabara yote. Kuna haja ya kujikita katika kuboresha elimu, hali ya uchumi wa raia wanaoathirika kwa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kwa upande mwingine, ni lazima kuongeza nguvu na kuweka juhudi zaidi katika vikosi vya ulinzi na usalama, kuwa wawazi na wakweli na kuhamasisha utu wema kwa nchi hifadhi za wahamiaji na wakimbizi. Hii iende sambamba na uangalifu mkubwa wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaofanyika ndani ya kila nchi. Mkutano wa kikundi cha Mtakatifu Martha, umetambua pia mchango mkubwa unaotolewa na wanaharakati wa kimataifa, uanzishwaji wa sekta binafsi na uwazi unaokuwepo katika ushirkiano wa kupiga vita biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kuna mafanikio makubwa yamefikiwa mpaka sasa lakini changamoto bado zipo.

Changamoto kubwa ambayo kikundi cha Mtakatifu Martha inakabiliana nayo kwa sasa, ni ule uwazi katika kushirikisha vyombo vya habari, ili jamii iweze kufahamu vema kazi iliyotendeka mpaka sasa na mpango mkakati wa miaka kadhaa kwa siku za usoni. Mfano mzuri wa ushirikiano wa namna hii ni huko nchini Uingereza, ambako Kanisa na vyombo vya ulinzi na usalama, wameshirikiana na vyombo vya habari ili kuhamasisha jamii na kuwawezesha watu kuchunguza na kutoa mapendekezo juu ya kupambana na hatimaye kutokomeza kabisa janga hili la biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Ushirikiano huo mahususi nchini Uingereza upo chini ya uongozi wa Kardinali Vincent Nichols, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikundi cha Mtakatifu Martha, na Askofu mkuu wa Westminster.

Katika hotuba yake kwa Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa mkutano wa kikundi cha Mt. Martha, Kardinali Vincent Nichols, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa juhudi zake za maneno na matendo zinazoweka bayana lengo dhahiri la Kanisa kuwa ni lile la kuzingatia utu na heshima ya binadamu, vinavyofumbatwa katika huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu, mintarafu hali ya maisha bora kwa kila binadamu.

Kardinali Nichols anasema, Kikundi cha Mtakatifu Martha Kimataifa, kimejitosa kwa ushirikiano na mshikamano mkubwa kuhakikisha kwamba, kinaamsha uelewa na kujenga uwajibikaji wa watu mahalia kila nchi, lakini zaidi ushirikiano wa kimataifa kuhakikisha janga hili la biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo inatokomezwa kutoka uso wa dunia. Kwa upande mwingne, Kardinali Nichols, kamuomba Baba Mtakatifu Francisko kuendelea kuhamasisha viongozi wa serikali, Taasisi za fedha na biashara, pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha wanafanya kila lililo ndani ya uwezo wao ili kutenda kwa utu wema katika kujibu kilio cha janga hili linalonyanyasa utu, heshima na haki msingi za binadamu!

Na Padre Celestine Nyanda.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.