2018-02-19 08:28:00

Papa Francisko: Zingatieni: kufunga, kusali na Neno la Mungu!


Injili ya Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka B wa Kanisa inakazia pamoja na mambo mengine: vishawishi, toba na wongofu wa ndani pamoja na Habari Njema ya Wokovu. Kristo Yesu kabla ya kuanza utume wake wa hadhara ulimwenguni, alijiandaa kwa muda wa siku arobaini kwa kusali na kufunga. Hakuwa na sababu ya kutubu na kuongoka, lakini kwa kuwa ni Neno wa Mungu aliyetwaa mwili kama binadamu, alipaswa kupitia majaribu haya kwa ajili yake Mwenyewe, lakini zaidi kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa milele na hatimaye, kuwajalia waja wake nguvu ya kuweza kushinda vishawishi.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 18 Februari 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Mjini Vatican wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana. Amesema, maandalizi ya utume wa Yesu hadharani yalijikita kwa namna ya pekee, katika mapambano ya maisha ya kiroho ili kuweza kumshinda Ibilisi. Kwaresima kwa waamini ni kipindi cha mapambano ya maisha ya kiroho! Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kusimama kidete dhidi ya Ibilisi kwa njia ya Sala, ili kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, waweze kumbwaga chini Ibilisi katika maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, dhambi na ubaya wa moyo ni mambo yanayoendelea kutendeka katika maisha ya watu. Matokeo yake ni vita na ghasia; vitendo vya ubaguzi, ubinafsi na hali ya mtu kujifungia katika undani wake bila kusahau ukosefu wa haki ndani ya jamii. Matendo yote haya ni kazi ya Ibilisi, baba wa maovu duniani. Yesu baada ya kujaribiwa na Ibilisi jangwani, alishuka na kuanza kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayomtaka mwamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa njia ya imani.

Kristo Yesu anatangaza kwamba, muda umetimia na Ufalme wa Mungu umekaribia, kumbe, ni wakati wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Binadamu wanapaswa kutambua kwamba, Ufalme wa Mungu upo kati yao na kuwa wanapaswa kumwongokea Mungu kila siku ya maisha yao. Hii ndiyo dhamana na wajibu unaotekelezwa na Mama Kanisa, kwani binadamu daima anakabiliwa na kishawishi cha kutaka kukimbilia mbali na uwepo wa Mungu, kumbe, waamini wanahamasishwa kuelekeza akili na nyoyo zao kwa Mwenyezi Mungu, kwa kujizatiti kikamilifu katika njia inayokwenda kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuambata na kuchuchumilia tunu msingi za maisha ya kiroho.

Vinginevyo, anasema Baba Mtakatifu, mwamini anaweza kupoteza dira na mwelekeo sahihi wa maisha kwa kuvutwa sana na malimwengu yanayofumbatwa katika ubinafsi. Waamini wanapaswa kujiaminisha na kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kutekeleza mapenzi yake na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha mradi wake wa upendo kwa kila mmoja wao. Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaotekelezwa katika hali ya furaha na unyofu wa moyo! Hiki si kipindi cha majonzi wala maombolezo. Ni dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa moyo wa furaha na uwajibikaji mkubwa kwa kuondokana na ubinafsi pamoja na kutupilia mbali utu wa zamani, kwa kujipyaisha na neema ya Sakramenti ya Ubatizo, ili hatimaye, kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha! Mwamini ataendelea kupoteza muda kwa kutafuta furaha katika mambo ya dunia; katika utajiri na mali; nguvu au weledi katika kazi. Ufalme wa Mungu ni utekelezaji makini wa matamanio halali ya binadamu, kwani huu ni wokovu wa binadamu na utukufu wa Mungu. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko kwa waamini kusikiliza kwa makini na kupokea kwa ari na moyo mkuu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani pamoja na kuiamini Injili. Huu ni mwanzo wa hija ya maisha ya kiroho, kuelekea katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, ili hatimaye, kuweza kupokea neema ya Mungu inayopania kuleta mabadiliko ulimwenguni ili kweli dunia iweze kusimikwa katika ufalme wa haki, amani na udugu.

Baba Mtakatifu, mwishoni mwa tafakari yake, anapenda kuwaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia kukiishi Kipindi cha Kwaresima, kwa kuwa waaminifu kwa Neno la Mungu;  na kwa kudumu katika Sala bila kuchoka kama alivyofanya Kristo Yesu, jangwani kwa muda wa siku arobaini. Mambo haya yanawezekana kabisa, kinachotakiwa ni kuwa na hamu ya kutekeleza upendo wa Mungu katika maisha; upendo unaopania kubadilisha maisha ya waamini na ulimwengu katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.