2018-02-19 14:01:00

Askofu Peter Ebere Okpaleke ang'atuka madarakani Jimbo la Ahiara!


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara, lililoko nchini Nigeria. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Lucisius Iwejuru Ugorji wa Jimbo Katoliki Umuahia, Nigeria kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Ahiara ambalo kwa sasa liko wazi! Itakumbukwa kwamba, Askofu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara aliteuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2012, lakini hakufanikiwa kuingia na kuongoza, kufundisha wala kuwatakatifuza waamini wa Jimbo Katoliki Ahiara kutokana na mgomo baridi uliotishwa na baadhi ya wakleri kwa madai kwamba, Kanisa lilitaka kuwakandamiza wananchi wa Ahiara. Hizi ni tuhuma ambazo hazikuwa na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Jimboni humo.

Baada ya kutafakari kwa kina kuhusu sakata hili, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Juni 2017 akawaandikia wakleri barua akiwataka kuonesha utii na kumkubali Askofu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara kwa maandizi katika kipindi cha siku 30 vinginevyo, wangefungiwa huduma ya kichungaji! Wakleri wakatekeleza amri hii lakini wakaonesha kwamba, ilikuwa ni kinyume kabisa cha utashi wao! Kanisa linaheshimu na kuthamini utashi wa mtu kama mahali patakatifu sana ambapo Mwenyezi Mungu anaongea na mwanadamu kutoka katika undani wa maisha yake! Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 19 Februari 2018 ameridhia kung’atuka kutoka madarakani kwa Askofu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara na Askofu Lucisius Iwejuru Ugorji wa Jimbo Katoliki Umuahia, sasa ameteuliwa kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Ahiara ambalo liko wazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.