Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Askofu Mkuu Ruwaichi: Ujumbe wa Kwaresima 2018 umefifishwa sana!

Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi asema, kuna baadhi ya vyombo vya habari vimefifisha ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2018 ili kuligombanisha Kanisa na Serikali. - RV

19/02/2018 09:29

Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2018. Hiki ni kipindi cha kujitafakari mbele ya Mungu na kufanya toba hususan uhai wa imani yetu kwa njia ya matendo ya huruma, haki, upendo na amani kwa jirani zetu, ni kipindi chenye upekee wa aina yake kwa sababu kuu tatu: Mosi,  ni katika mwaka huu ambapo Kanisa Katoliki Tanzania  linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, na kilele chake kitakuwa tarehe 2 Oktoba 2018.

Pili, Mwaka huu pia utakuwa ni mwaka wa 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko rasmi kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi yetu; na tatu Mwaka huu ni mwaka wa maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji  hapo mwakani 2019. Kwa sababu kuu hizo tatu, ni vema tafakari yetu ya Kwaresima ikalenga katika swali ambalo, kwa namna moja au nyingine, linahusu sababu hizo tatu. Kwa njia ya swali hilo mwanadamu hudiriki kumhoji na kumuuliza Mungu na Muumba wake kuhusu hali ya binadamu mwenzake. Swali hilo ni “Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mw. 4:9).

Katika mahojiano maalum na Vatican News, Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya vyombo vya habari ndani na nje ya Tanzania vilivyopotosha kwa makusudi kabisa Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Ujumbe wa Kwaresima umezingatia mambo makuu matatu yaliyobainishwa kwenye utangulizi wake kwa kujikita katika kauli mbiu “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu “. Wakristo wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika mazingira yenye changamoto nyingi.

Askofu Mkuu Ruwaichi anasikitika kusema baadhi ya vyombo vya habari vimeufifisha ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa kusema kwamba, ni tamko la kuishambulia serikali iliyoko madarakani. Habari hizi si sahihi wala kweli. Lengo msingi la ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ni kukoleza moyo wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni ujumbe kwa watu wa Mungu na watu wote wenye mapenzi mema nchini Tanzania.

Baraza la Maaskofu linaialika familia ya Mungu nchini Tanzania kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu katika maisha yao; kuitafakari na kuiishi. Wakristo kwa namna ya pekee, wanahimizwa kadiri ya nafasi, vipaji na majukumu yao kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha. Ni nia ya Maaskofu kutaka kutekeleza sauti yao ya kinabii kwa kusimamia: Ukweli, kwa kuonya, kuombea na kutakasa sanjari na utekelezaji wa dhamana yake ya kitume kwa kuwaalika watanzania wte kutazama hali yao halisi katika nyanja za: kijamii, kisiasa, kiuchumi, kimaadili nk.  Ili hatimaye kuifanyia kazi katika hali inayompendeza Mwenyezi Munguna kuchangia katika kuleta tija, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Tanzania. Kuna changamoto, lakini pia kuna mafaanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana nchini Tanzania. Yote haya yatazamwe kwa dhati kabisa na kufanyiwa kazi katika mwanga wa ukweli kwa msingi wa haki, kwa kuheshimu uhai, uhuru na heshima ya kila raia wa Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

19/02/2018 09:29