Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Kung'oka kwa Jacob Zuma uwe ni mwanzo wa sheria kushika mkondo wake

SACBC linasema, uchunguzi wa kina ufanyike dhidi ya Bw. Jacob Zuma, ili ukweli ufahamike, sheria ichukue mkondo wake na haki kutendeka. - EPA

18/02/2018 07:30

Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 75 aliyeshinikizwa na Chama cha A.N.C kung’atuka kutoka madarakani tarehe 14 Februari 2018, tangu alipoingia madarakani kunako mwaka 2009 alikuwa akikabiliwa na shutuma za rushwa na ufisadi wa dola milioni 24 kwa ajili ya kukarabati makazi binafsi huko Nkandla; ubakaji alioufanya kunako mwaka 2006: pamoja na kashfa ya biashara haramu ya silaha. Haya ni makossa mazito ambayo yasingaliweza kumwacha salama Bwana Jacob Zuma. Lakini kubwa zaidi ni tuhuma za rushwa na ufisadi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, (SACBC), limempongeza Rais Mstaafu Jacob Zuma kuwa kuamua kung’atuka kutoka madarakani na kwamba, hii ni hatua kubwa kwa Afrika ya Kusini kuanza mchakato wa kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kwa kuzingatia: utawala wa sheria, kanuni maadili na utu wema, ili hatimaye, Afrika ya Kusini iweze kurejesha heshima yake kimataifa; kwa kufufua uchumi shirikishi unaowajali maskini na wanyonge ndani ya Afrika ya Kusini.

Hii ni sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Askofu mkuu Stephen Brislin, Rais wa Baraza la Maaskofu Afrika ya Kusini. Maaskofu wanavishauri vyombo vya sheria kuhakikisha kwamba, vinafanya uchunguzi wa kina juu ya shutuma za rushwa na ufisadi zinazomkabili Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini Bwana Jacob Zuma, ili ukweli uweze kufahamika, sheria kushika mkondo wake na haki kutendeka. Lengo ni kuhakikisha kwamba, vitendo vya rushwa na ufisadi nchini Afrika ya Kusini vinakomeshwa! Itakumbukwa kwamba, familia ya Mungu nchini Afrika ya Kusini Mwaka 2018 inaadhimisha Jubilei ya Kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu Mzee Nelson Madiba Mandela alipozaliwa. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini kwamba, Mzee Madiba, ataendelea kuwa mfano bora wa kuigwa kwa wananchi wengi wa Afrika ya Kusini katika kutetea misingi ya haki, amani, usawa, demokrasia na utawala wa sheria.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kumwombea Rais Cyril Ramaphosa, aliyeapishwa rasmi tarehe 15 Februari 2018 ili aweze kutenda kazi zake kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Muda wake wa uongozi unatarajiwa kukamilika kunako mwaka 2019, Afrika ya Kusini, itakapoingia tena kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu.  Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini kwamba, wataweza kutumia Kipindi hiki cha Kwaresima kwa ajili ya kusali, kufunga, kutubu na kulitafakari Neno la Mungu ambalo linapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha yao, tayari kuadhimisha Injili ya matumaini inayofumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

18/02/2018 07:30