Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maendeleo

Wahudumu wa afya wawe ni mashuhuda wa huruma, imani na mapendo!

Wahudumu wa sekta ya afya wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo, imani na matumaini kwa wagonjwa wanaowahudumia. - REUTERS

17/02/2018 07:10

Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, Kenya katika maadhimisho ya Siku ya XXVI ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2018, amewataka wahudumu wa sekta ya afya kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma, upendo na imani wakati wote wanapowahudumia wagonjwa na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Bikira Maria, Mama wa huruma awe ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa wagonjwa. Imani iwasaidie wahudumu katika sekta ya afya kuonja shida na mahangaiko ya jirani za, tayari kumkaribia Kristo Yesu aliyeteseka, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu! Huyu ndiye Kristo Yesu anayeendelea kuteseka pamoja na wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Njue, amewataka waamini kukimbilia ulinzi na tunza kwa Bikira Maria, ili aweze kuwaangalia kwa jicho lenye huruma na mapendo kama ilivyokuwa kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake hapa duniani. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, anaadhimisha Siku ya Wagonjwa Duniani. Huu ni muda muafaka wa kusali na kutafakari kuhusu Fumbo la Mateso na Mahangaiko katika maisha ya binadamu na matumaini yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, alama ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ni siku muafaka ya kuwasaidia wagonjwa katika shida na mahangaiko yao ya kila siku sanjari na kuhakikisha kwamba, haki zao msingi, utu, heshima yao vinalindwa. Jamii ihakikishe kwamba, wagonjwa wanapata mahitaji yao muhimu kama kielelezo pia cha upendo na mshikamano kwani upendo ni kiini cha Injili ya Kristo!

Wakati huo huo, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika maadhimisho ya Siku ya XXVI ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2018 amesema, waamini pamoja na wahudumu katika sekta ya afya hawana budi kujifunga kibwebwe ili: kuwahudumia, kuwafariji, kuwapunguzia au kuwaondolea maumivu wagonjwa na pale inaposhindikana kuwasindikiza katika safari yao ya mwisho hapa duniani, daima wakikumbushwa kwamba, wao ni wasafari na hapa duniani hawana makazi ya kudumu: Wakristo wanatumaini katika maisha ya uzima wa milele. Mwanadamu katika maisha yake hapa duniani, anakabiliwa na magonjwa ya kiroho, kimwili, kiutu, lakini zaidi kimaadili yanayodhohofisha mwili na kuathiri maisha ya kiroho na kiutu! 

Fumbo la mateso anasema Kardinali Gualtiero Bassetti ni sehemu ya historia ya maisha ya binadamu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alilikabili Fumbo la Mateso kwa amani, utulivu na upendo mkuu kwani kwa njia hii alikuwa anatekeleza kazi ya ukombozi na utashi wa Baba yake wa mbinguni. Kumbe, utume kwa wagonjwa ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Huduma makini inayotolewa kwa wagonjwa majumbani na hospitalini ni ushuhuda wau pendo endelevu wa Kristo kwa waja wake.

Dhamana hii inapaswa kutambuliwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoheshimu Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wakleri, watawa, waamini walei pamoja na wahudumu wa sekta ya afya watambue kwamba, huu ni utume muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, mwendelezo wa kazi iliyoanzishwa na Kristo Yesu ili kuganga na kuwaponya watu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Kardinali Gualtiero Bassetti anawaalika vijana kujenga na kudumisha utamaduni wa huduma kwa wagonjwa na maskini kwa kujinyima sehemu ya muda wao wa starehe ili kujichotea neema na baraka katika maisha kwa njia ya huduma makini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

17/02/2018 07:10